Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Mheshimiwa Japhari Kubecha, amefanya kikao maalum na wazee wa Tanga Asili ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa mikutano ya kusikiliza maoni na ushauri kutoka kwa wazee kuhusu mustakabali wa maendeleo ya wilaya hiyo. Kikao hicho kililenga kukuza ushirikiano kati ya serikali na kundi hili muhimu katika jamii.
Katika mazungumzo yake na wazee hao, DC Kubecha alisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wazee katika kutoa ushauri kwa viongozi mbalimbali wa wilaya. Alieleza kuwa hekima na uzoefu wa wazee ni hazina kubwa inayoweza kusaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.
Mhe. Kubecha aliwataka wazee hao kuhakikisha kuwa kila kata kati ya 27 zilizopo wilayani Tanga inakuwa na angalau viongozi watano wa wazee. Alisema lengo ni kuwajumuisha wazee hawa katika shughuli za serikali kuanzia ngazi ya chini kabisa hadi mtaa, ili waweze kutoa ushauri wa karibu na kuimarisha utawala bora.
Kwa kuhitimisha, DC Kubecha alisisitiza kuwa mchango wa wazee wa Tanga Asili ni muhimu katika kuendeleza ajenda ya maendeleo na kuitangaza Tanga kama lango kuu la uchumi wa Afrika Mashariki. Kauli mbiu ya kikao hicho ilikuwa: “Tanga Yetu, Lango la Uchumi wa Afrika Mashariki.”