Na. Jacob Kasiri – Njombe.
Wakati zoezi la kuzipigia kura Hifadhi za Taifa 10 zilizoingia katika kinyang’anyiro cha kuwania tuzo mbalimbali ikiwemo tuzo ya Eneo Bora la Fungate Barani Afrika (Africa’s Leading Honeymoon Destination) likiendelea katika mikoa mbalimbali Tanzania bara na Visiwani linajulikana kama *VoteNow* limevutia hisia na kuleta hamasa kwa wananjombe ambapo zaidi kura 330 Kutoka Wilaya ya Makete zimepigwa na kuiweka TANAPA katika nafasi nzuri ya kunyakua Tuzo hizo.
Tuzo hizo za utalii zinazotolewa na Taasisi ya *The World Travel Awards* yenye Makao yake Makuu jijini London nchini Uingereza zinafaida kubwa kwa Wizara ya Maliasili na Utalii, taasisi husika na Taifa kwa ujumla kwani tuzo hizo zinazifanya Hifadhi za Taifa zilizoshinda kujulikana kimataifa na kuongeza idadi ya watalii watakaotembelea hifadhi hizo.
Wapigisha kura hao kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wakiongozwa na Afisa Mwandamizi na Mkuu wa Kitengo cha Utalii, Hifadhi ya Taifa Ruaha Amina Salum walifarijika kwa mwitikio huo wa Watanzania wengi hususani wakazi wa mji wa Njombe na viunga vyake kwa kujitokeza na kupiga kura hizo ambazo zitaongeza idadi ya kura katika kinyang’anyiro hicho kinachohusisha mataifa mbalimbali barani Afrika yenye vivutio vyenye hadhi na sifa kama tulivyonavyo Tanzania.
Akiwapokea Maafisa na Askari hao kutoka TANAPA, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete Dkt. Ligobert Kalisa alisema, “Watanzania lazima tuunganishe nguvu zetu na Njombe iwe mfano kwani Hifadhi mbili za Kitulo na Ruaha zimo kwenye kinyang’anyiro, hivyo ushindi wa Hifadhi hizo ni heshima kwa Taifa na Mkoa wetu wa Njombe.”
Aidha, Dkt. Kalisa aliongeza kuwa watanzania tumuunge mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia filamu mbili na diplomasia anayoifanya kimataifa kwa kuzipigia kura Hifadhi za Taifa 10 zinyakue tuzo hizo mujarabu.
Naye, Afisa Mwandamizi na Mkuu wa Kitengo cha Utalii, Hifadhi ya Taifa Ruaha Amina Salum alisema kuwa lengo la ujio wao mkoani Njombe ni kuhamasisha zoezi la kupiga kura ili hifadhi hizo zishinde, hata hivyo aliendelea kuwasisitiza wananjombe kutembelea Hifadhi za Taifa Ruaha na Kitulo kwani gharama ya viingilio ni nafuu na wao ndio wako karibu na vivutio hivyo.
Timu hiyo inayoongoza zoezi la “VoteNow”iliyowasili mjini Njombe Aprili 22, 2025 imeshapigisha Kura katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Makete, Ofisi ya Mkurungezi na Idara na Vitengo vyake, Chuo cha VETA – Makete na Chuo cha Ualimu Tandala,na Zoezi hilo bado linaendelea.