DAR ES SALAAM, Aprili 2025
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma, amesema kuwa mlundikano wa mashauri katika Mahakama ya Rufani ni changamoto kubwa inayoikabili Mahakama hiyo kwa sasa.
Ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Mahakama ya Rufani uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake ya ufunguzi, Jaji Mkuu alibainisha kuwa kwa mwaka 2024, Mahakama ya Rufani ilikuwa na jumla ya mashauri ya mlundikano 1,273, sawa na asilimia 21 ya mashauri yote katika Mahakama hiyo, na kuchangia asilimia 74 ya mlundikano wa mashauri katika ngazi zote za Mahakama nchini.
Ngazi nyingine za Mahakama zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti tatizo hilo. Kwa mfano, Mahakama Kuu ilikuwa na asilimia 2 tu ya mashauri ya mlundikano, Mahakama za Hakimu Mkazi asilimia 6, Mahakama za Wilaya asilimia 1, huku Mahakama za Mwanzo zikiwa hazina mlundikano kabisa.
“Hali hii inatufanya tuone dhahiri kuwa Mahakama ya Rufani ina mzigo mkubwa zaidi wa mashauri, jambo linalotufanya tuangalie upya taratibu na mifumo yetu ya kazi,” alisema Jaji Mkuu Profesa Juma.
Akizungumza kuhusu mikakati ya kupunguza tatizo hilo, alieleza kuwa Mkuu wa Idara ya TEHAMA kwa kushirikiana na Wakala wa Serikali Mtandao (eGA) atawasilisha mada kuhusu “Matumizi ya TEHAMA katika usikilizaji wa Mashauri/Business Process Re-engineering ya Mahakama ya Rufani.” Mada hiyo inalenga kuchochea matumizi ya teknolojia ili kuboresha utendaji wa Mahakama hiyo.
Jaji Mkuu alieleza kuwa sababu kuu mbili zinazochangia ongezeko la mashauri katika Mahakama ya Rufani ni pamoja na upanuzi mkubwa wa huduma za Mahakama Kuu nchini—ambapo ifikapo mwisho wa mwaka 2025 ni Mkoa wa Pwani pekee utakaokuwa haujapata jengo la Mahakama Kuu—na matumizi ya mifumo ya TEHAMA kama JoT-eCMS, Video Conference, na udijitali wa nyaraka, ambayo imeongeza ufanisi katika Mahakama za ngazi za chini.
Hata hivyo, alionya kuwa matumizi ya teknolojia katika Mahakama ya Rufani, hususan Video Conference, bado ni madogo ukilinganisha na Mahakama nyingine. Alisisitiza kuwa ni lazima Mahakama hiyo ijiandae kwa mabadiliko ya kina kupitia Business Process Reengineering na kuanza kutumia teknolojia ya Artificial Intelligence na Machine Learning ili kukabiliana na wingi wa mashauri.
Katika mkutano huo, viongozi wa Mahakama walikubaliana kuwa ni muhimu kupitia upya sheria, kanuni na taratibu mbalimbali ili kuongeza ufanisi wa utoaji haki na kupunguza mlundikano wa mashauri.
Jaji Mkuu pia aligusia mafanikio aliyoyashuhudia katika Mkutano wa Majaji Wafawidhi uliofanyika Februari 2025 jijini Mwanza, ambapo alielezwa kuwa tayari kuna matumaini ya kupunguza muda wa kutambua mlundikano wa mashauri kutoka miezi 12 hadi miezi nane au hata sita.