

Mkuu wa Mafunzo Peak Performance International ,Tanzania Ikunda Kisamo akizungumza jambo wakati akifundisha wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, Kituo cha Upanga .

Mkuu wa Kitengo cha Kozi Fupi,Ubunifu na Shauri za Kitaalamu, Dkt. Darlene Mutalemwa akizungumza na wanafunzi wa Chuo hicho wakiwa katika mafunzo maalum kwa ajili ya kuwaongezea ujuzi katika maeneo mbalimbali ikiwemo mapinduzi ya ujasiriamali na matumizi ya teknolojia ya kisasa.




Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, Kituo cha Upanga wakiwa katika mafunzo maalum kwa ajili ya kuongezea ujuzi katika maeneo mbalimbali ikiwemo mapinduzi ya ujasiriamali na matumizi ya teknolojia ya kisasa.
…….
Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam kimeendesha mafunzo maalum kwa wanafunzi wa Ndaki hiyo kwa lengo la kuwaongezea ujuzi katika maeneo mbalimbali ikiwemo mapinduzi ya ujasiriamali, matumizi ya teknolojia ya kisasa pamoja na mbinu bora za kuwashawishi waajiri ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika Kituo Ndaki hiyo Upanga , Mkuu wa Mafunzo Peak Performance International ,Tanzania Ikunda Kisamo amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwaandaa washiriki kukabiliana na ushindani wa soko la ajira kimataifa kwa kuwajengea uwezo wa kiubunifu na kuongeza tija katika utendaji wao.
“Waajiri wa sasa wanahitaji wafanyakazi wenye uwezo wa kufanya zaidi ya majukumu ya kawaida, wenye ubunifu na wanaotumia teknolojia kuongeza ufanisi,” amesema Kisamo.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamewapa washiriki mbinu za kuwashawishi waajiri kutoka mataifa mbalimbali kwa kuonyesha uwezo na maarifa ya kipekee.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Kozi Fupi,Ubunifu na Shauri za Kitaalamu, Dkt. Darlene Mutalemwa, amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuongeza uelewa wa wanafunzi kuhusu mahitaji halisi ya soko la ajira na namna bora ya kuyakidhi kwa ufanisi.
“Washiriki walipata nafasi ya kubadilishana uzoefu na mkufunzi, jambo ambalo linaongeza maarifa na kuimarisha utendaji wao katika maeneo mbalimbali,” amesema Dkt. Mutalemwa.
Wanafunzi na aadhi ya wafanyakazi walioshiriki wameeleza kufurahishwa kwao na mafunzo hayo, huku wakisema kuwa yamekuja wakati muafaka ambapo dunia inahitaji watu wenye maarifa ya kisasa na uwezo wa kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia.
“Katika dunia ya sasa, teknolojia ina nafasi kubwa katika mafanikio ya kazi yoyote. Mafunzo haya yamenipa mwanga mpya wa namna ya kuongeza ufanisi wangu,” amesema Rebeca John, mwanafunzi wa Chuo hicho.
Uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam umeahidi kuendelea kutoa mafunzo ya aina hiyo mara kwa mara ili kusaidia katika kujenga jamii yenye maarifa na uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika sekta mbalimbali.