Waziri wa Afya Mhe.Jenista Mhagama,akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 25,2025 wakati wa Siku ya Malaria Duniani.
Waziri wa Afya Mhe.Jenista Mhagama,akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 25,2025 wakati wa Siku ya Malaria Duniani.
Waziri wa Afya Mhe.Jenista Mhagama,akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 25,2025 wakati wa Siku ya Malaria Duniani.
Na.Alex Sonna-DODOMA
Dunia ikiwa inaadhimisha siku ya Malaria, nchini Tanzania takwimu zinaonesha kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kimepungua kwa takribani asilimia 45 kutoka asilimia 14.8 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2022.
Takwimu hizo zinaonesha Mkoa wa Tabora unaongoza kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya Malaria kwa asilimia 23, ukifuatiwa na Mkoa wa Mtwara wenye kiwango cha maambukizi asilimia 20, Kagera asilimia 18, Shinyanga asilimia 16 na Mkoa wa Mara wenye asilimia 15.
Hayo yameelezwa leo Aprili 25,2025 na Waziri wa Afya Jenista Mhagama wakati akizungumza na waandishi wa habari na kufafanua kuwa mikoa yenye kiwango cha chini cha maambukizi ya malaria kwa chini ya asilimia moja ni Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Dodoma, Songwe, Mwanza, Dar Es Salaam, Iringa, na Singida.
Amesema katika utekelezaji wa mikakati na afua mbalimbali za kupambana na ugonjwa wa Malaria hapa nchini
idadi ya wagonjwa waliothibitika kuwa na malaria imepungua kwa asilimia 45 kutoka wagonjwa milioni 6.0 mwaka 2020 hadi kufikia wagonjwa milioni 3.3 kwa mwaka 2024.
“Aidha idadi ya wagonjwa wanaolazwa kutokana na malaria kwa asilimia 33 imepungua kutoka wagonjwa 306,633 kwa mwaka 2020 hadi kufikia wagonjwa 206,453 mwaka 2024 na kupungua kwa idadi ya vifo vitokanavyo na ugonjwa wa malaria kwa asilimia 39 Kutoka vifo 2,460 kwa mwaka 2020 hadi kufikia vifo 1503 kwa mwaka 2024,”ameeleza
Waziri Mhagama amefafanua kuwa kuongezeka kwa Mikoa yenye kiwango cha maambukizi ya malaria chini ya asilimia moja, kutoka mikoa 5 mwaka 2020 hadi kufikia mikoa 6 kwa mwaka 2024 na kutoka Halmashauri 36 mwaka kwa 2020 hadi kufikia Halmashauri 51 kwa mwaka 2024.
Ameitaja Mikoa hiyo kuwa ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Singida, Dodoma, Songwe, Iringa, Dar es Salaam na Mwanza.
“Tumeimarisha pia upatikanaji wa huduma za kupima ugonjwa wa malaria kwa kutumia kipimo kinachotoa majibu kwa haraka (mRDT) na dawa za kutibu malaria kwenye vituo vyote vya kutolea huduma za Afya na kuimarika kwa upatikanaji wa dawa na bidhaa muhimu za malaria kwenye vituo vyote vya umma vya kutolea huduma ambapo upatikanaji wa bidhaa hizo ni zaidi ya asilimia 90,”amesisitiza.
Katika kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma za Malaria hapa nchini Waziri huyo amesema Wizara, imeimarisha na kuongeza msisitizo wa utekelezaji wa mikakati na
afua zote za kupambana na malaria huku Msisitizo mkubwa ukiwekwa kwenye uwekezaji katika udhibiti wa mbu waenezao malaria kwa njia jumuishi ikiwemo kutoa kipaumbele katika afua ya usimamizi na udhibiti wa mazingira.
“Wizara yangu pia imeendelea kushirikiana na Baraza la Kutokomeza Malaria Tanzania, lililoundwa mwaka 2022, kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya kupambana na ugonjwa wa malaria nchini,
Hali hiii itaziba pengo la upungufu wa rasilimali ambalo kwa sasa ni takribani asilimia 56. Baraza hili, linaloongozwa na Mhandisi. Leodegar Tenga, linaendelea kuhamasisha upatikanaji wa rasilimali hizo kupitia sekta mtambuka ikiwemo sekta binafsi, Asasi za Kijamii na Taasisi za Kidini, “amesema
Kwa upande wa bidhaa za uchunguzi na tiba ya malaria, amesema Wizara kupitia Bohari Kuu ya Dawa – MSD imeendelea kuhakikisha vituo vyote vya umma vya kutolea huduma za Afya hapa nchini vinapata dawa za malaria na
vitendanishi vya kutosha na kwa wakati ambazo hutolewa bila malipo kwa wananchi.
Siku ya Malaria Duniani, huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Aprili ambapo katika siku hii, Tanzania huungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha kumbukumbu ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria.
Aidha, siku hii inalenga katika kutathmini utekelezaji wa mikakati na afua za za kudhibiti ugonjwa wa malaria, mafanikio yaliyopatikana kutokana na jitihada za Serikali na wadau, pamoja na changamoto zilizopo na jinsi ya kukabiliana nazo.
Siku hii pia hutumika kutoa elimu na hamasa zaidi kwa jamii juu ya afua pendekezwa na wajibu wa makundi mbalimbali katika kupambana na malaria hapa nchini na Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya mwaka huu inasema “Malaria Inatokomezwa na Sisi: Wekeza, Chukua Hatua – Ziro Malaria Inaanza na Mimi.”