Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Peter Msofe, akitembelea mabanda ya wabunifu wakati wa maonesho ya Wiki ya Ubunifu ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), yaliyofanyika leo Aprili 25, 2025, katika ukumbi wa chuo hicho jijini Dar es Salaam
…….
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imedhamiria kuimarisha mazingira ya ubunifu nchini, hususan katika sekta ya afya, kwa kutoa mchango wa rasilimali kwa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS). Hatua ambayo inalenga kuchochea maendeleo ya suluhisho za kisasa zinazoweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikumba jamii.
Akizungumza leo Aprili 25, 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga maonesho ya Wiki ya Ubunifu ya kwanza ya MUHAS, kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Prof. Carolyne Nombo, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Profesa Peter Msofe, amesema kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono bunifu zinazozaliwa ndani ya vyuo vikuu hususan MUHAS, kwa kuwa ubunifu ni silaha muhimu ya kutatua changamoto katika sekta ya afya na maeneo mengine ya kijamii.
“Serikali itaendelea kuwa mshirika wa karibu wa MUHAS ambazo zimeweka ubunifu kama sehemu ya vipaumbele vyake. Afya ya mwanadamu ni suala mtambuka na linahitaji suluhisho mpya kila wakati kutokana na mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na kiteknolojia,” amesema Prof. Msofe.
Ameongeza kuwa Wiki ya Ubunifu ya MUHAS imekuwa jukwaa muhimu la kuthibitisha kuwa vijana wa kitanzania wanaweza kubuni na kutekeleza mawazo ya mabadiliko kwa manufaa ya jamii.
Amesema kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia itahakikisha kuwa wiki kama hizo zinapewa kipaumbele na zinaungwa mkono ili kuibua vipaji vipya.
“Ubunifu sio tukio la maadhimisho pekee bali ni mchakato unaopaswa kuingizwa katika mfumo mzima wa utoaji elimu nchini. Tunaamini kuwa kupitia wiki kama hii, vijana na watafiti watahamasika zaidi kuja na suluhisho mbadala za matatizo yetu,” amesema Prof. Msofe.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa, amesema kuwa chuo hicho kimejipanga kuhakikisha kuwa ubunifu hauishii darasani bali unatafsiriwa kwa vitendo kwa faida ya jamii.
Profesa Kamuhabwa amesema kuwa MUHAS tayari kimeanzisha Kitengo cha Ubunifu na Kituo cha Ukuaji wa Ubunifu (Innovation Hub) katika Kampasi ya Mloganzila ili kuratibu na kuendeleza mawazo ya wabunifu kutoka ndani ya chuo hicho.
“Tumeshuhudia bunifu zinazolenga kutatua changamoto katika uchunguzi wa magonjwa, utengenezaji wa dawa za gharama nafuu, kuboresha vifaa tiba, matumizi ya bidhaa asilia kwa njia salama na za kitaalamu. Tunataka bunifu hizi zifike kwa wananchi na kuleta mabadiliko ya chanya” amesema Prof. Kamuhabwa.
Amesema kuwa MUHAS kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, wakiwemo washirika kutoka Sweden, imeweza kuimarisha mifumo ya ubunifu ili kuendana na kasi ya mahitaji ya huduma bora za afya nchini.
Miongoni mwa wabunifu waliopata nafasi ya kuonesha kazi zao ni pamoja na mwanafunzi wa mwaka wa nne wa Udaktari kutoka MUHAS, Clara Mcharo, ambaye alibuni mfumo wa kiteknolojia wa kusaidia wakunga kuwahudumia akinamama wajawazito kwa wakati mmoja.
“Changamoto kubwa ni uwiano usio sawa kati ya wakunga na wagonjwa. Mfumo huu tulioleta unalenga kusaidia wakunga kuweza kufuatilia afya ya akinamama wanaojifungua kwa urahisi na haraka zaidi, na hivyo kupunguza hatari wakati wa kujifungua,” amesema Clara.
Wiki ya Ubunifu ya MUHAS, ambayo ilianza rasmi Aprili 22, 2025, imefanyika kwa mafanikio makubwa, ambapo wabunifu mbalimbali kutoka ndani ya chuo hicho walipata fursa ya kuonesha miradi yao ya ubunifu mbele ya wataalam, wadau wa afya, wahadhiri, wanafunzi na wananchi wa kawaida.
Maadhimisho hayo yameongozwa na kaulimbiu “Kuelekea Mustakabali wa Ubunifu katika Afya” ambapo yamelenga kujenga mazingira ya kuendeleza vipaji, kukuza ushirikiano kati ya wabunifu na taasisi, pamoja na kuchochea matumizi ya utafiti na ubunifu katika kuboresha huduma za afya.