Dkt. Ester Kibga, mkufunzi wa Chuo cha Aga Khan akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
KUTOKANA na juhudi za muda mrefu za Chuo cha Aga Khan kuhamasisha masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM), chuo hicho kwa sasa kinatoa mafunzo kwa walimu wa shule za msingi na sekondari za serikali na binafsi, ili kuwafikia walaji wakuu wa elimu ambao ni wanafunzi pamoja na walimu walioko mashuleni.
“Ni dhamira ya Chuo cha Aga Khan kuhakikisha walimu na wanafunzi wanashiriki kikamilifu katika ujifunzaji unaomhusisha mwanafunzi kwa vitendo zaidi,” walisema waandaaji wa mafunzo hayo.
Mafunzo haya yanawapa walimu mbinu mbalimbali za kufundishia ambazo zinamuwezesha mwanafunzi kujifunza kwa kutenda. Walimu wamefundishwa ujuzi mbalimbali unaosaidia kuibua maarifa kwa wanafunzi endapo mbinu bora zitatumika.
Kwa sasa, nyenzo zilizotumika katika mafunzo hayo hazihusishi tu somo la Fizikia bali pia zimepanuliwa kuhusisha masomo ya Kemia, Biolojia, Hisabati na Jiografia.
Kwa mujibu wa waandaaji wa mafunzo hayo, mbinu hizi mpya zinalenga kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji mashuleni, hasa kwa masomo ambayo mara nyingi yamekuwa magumu kwa walimu na wanafunzi kuyamudu.
Dkt. Ester Kibga, mkufunzi wa Chuo cha Aga Khan na mwezeshaji wa mafunzo hayo, alisema kuwa mafunzo hayo yamepata mwitikio mkubwa kutoka kwa walimu wa ngazi na taasisi mbalimbali, jambo linaloonesha uelewa mpana kuhusu umuhimu wa masomo ya STEM.
“Masomo ya STEM hayafundishwi kama masomo mengine mashuleni. Huko shuleni tunafundisha Sayansi, Kemia, Fizikia, Historia, Biolojia na Hisabati. Kupitia mafunzo haya, tunataka walimu waone umuhimu wa kuwafundisha watoto vizuri masomo haya kwa sababu ni ya msingi sana katika zama hizi za maendeleo ya teknolojia,” alisema Dkt. Kibga.
Aliongeza kuwa teknolojia ni nyenzo muhimu katika kuboresha ujifunzaji wa mwanafunzi kwa sababu hufanya masomo kuwa rahisi na ya kuvutia zaidi.
Kwa upande mwingine, Ameria Kianga kutoka benki ya DTB alieleza kuwa benki yao imevutiwa kudhamini mafunzo haya kwa kutoa msaada wa elimu ya kidigitali kwa walimu na wadau mbalimbali wa elimu.
“Kupitia mafunzo haya, tumetambua nafasi ya kuwaelimisha walimu kuhusu huduma zetu, ikiwemo utoaji wa mikopo bila kujaza fomu na kuwasaidia kuanzisha akaunti za watoto ili kuweka akiba kwa ajili ya malengo ya baadaye,” alisema Ameria.
Ameria pia alisisitiza umuhimu wa kuwaelimisha walimu na wanafunzi jinsi ya kutumia simu na kompyuta kwa njia za kidijitali na kujihudumia kibenki badala ya kutumia vifaa hivyo kwa michezo pekee.
Charles Maina Muigai, mwezeshaji wa mafunzo kutoka Aga Khan Mombasa, alisema kuwa amevutiwa na mtindo wa mafunzo kwa vitendo, unaowawezesha walimu kuelewa na kufundisha kwa ufanisi zaidi.
“Kwa kutumia Physics Education in Technology (PhET), nimeweza kupata ujuzi wa kuwaonesha walimu mambo kwa vitendo kwa ujasiri zaidi. Hii itawawezesha walimu wa Sayansi kujiandaa vizuri na kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuwafundisha wanafunzi wao,” alisema Muigai.
Aliongeza kuwa matarajio yake ni kuwaelimisha zaidi walimu anaowafundisha, ili nao waweze kuwahamasisha wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati.