OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa wito kwa Watanzania kuuenzi Muungano kwa ajili ya kudumisha amani, umoja na udugu huku akipendekeza kuanzishwa kwa wiki maalum ya Muungano kwa shule zote nchini ili kukuza uelewa wa wanafunzi kuhusu historia ya Muungano.
Mhe.Mchengerwa ameyasema hayo katika kijiji cha Sangambi mkoani Mbeya baada ya kukagua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi ya maendeleo yenye thamani ya Sh.bilioni 40 huku wananchi wakimpongeza Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa.
Amehamasisha wasanii na waandishi kuendeleza simulizi za mshikamano wa kitaifa ili kudumisha Muungano huku akiwaasa wazazi kuwaelimisha vijana juu ya thamani ya Muungano.
Amesisitiza kuwa Tanzania ni mfano wa amani barani Afrika, tofauti na mataifa mengine yaliyogubikwa na migogoro na kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulikuwa wa kweli, wa kiitikadi na kimaadili, na umeleta mafanikio makubwa kwa taifa.
Waziri Mchengerwa ampongeza Rais Samia kama alama ya mafanikio ya Muungano, akisema kuwa Tanzania imekuwa ya kwanza Afrika Mashariki kumpa mwanamke nafasi ya urais, jambo ambalo hata mataifa makubwa hayajafanikisha.