Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, wakiwa katika picha ya pamoja wakati wakishiriki bonanza maalum la michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa wavu, mpira wa ufukweni, draft, bao, karata na michezo ya ubunifu, lililofanyika leo Aprili 26, 2025 katika Fukwe za Empire, Bagamoyo, mkoani Pwani. Tukio hili ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mshikamano, afya na mahusiano bora kazini kwa ajili ya kuongeza tija katika utendaji wa majukumu yao ya kila siku. (PICHA NA NOEL RUKANUGA)

Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Biashara, Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es SalaamDkt. Joshua Mwakujonga (kushoto) akicheza mchezo wa draft na wafanyakazi wezake wa ndaki hiyo katika bonanza maalum la michezo mbalimbali lililofanyika leo Aprili 26, 2025 katika Fukwe za Empire, Bagamoyo, mkoani Pwani.
……
Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam wameungana kushiriki bonanza maalum la michezo lililofanyika katika Fukwe za Empire, Bagamoyo, Mkoani Pwani, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mshikamano, afya na mahusiano bora kazini kwa ajili ya kuongeza tija katika utendaji wa majukumu yao ya kila siku.
Bonanza hilo ambalo limefanyika katika siku ya kumbukizi ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, liliwaleta pamoja wafanyakazi wa Idara mbalimbali wakiwemo wahadhiri, watendaji wa utawala, ambapo wameshiriki michezo mbalimbali ya kufurahisha na kuchangamsha akili kama mpira wa wavu na ufukweni, draft, bao, karata na michezo ya ubunifu.
Akizungumza leo April 26, 2025 Mkoani Pwani, wakati wa Bonanza hilo, Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya Biashara, Dkt. Joshua Mwakujonga, amebainisha kuwa bonanza hilo limekuwa na faida kubwa kwa wafanyakazi kwa kuwa limesaidia kubomoa matabaka kazini na kujenga mahusiano ya karibu baina ya wafanyakazi wa kada mbalimbali.
“Mbali na kushiriki michezo, tumepata fursa ya kufanya mazoezi pamoja, kushiriki chakula na vinywaji kwa pamoja, yote haya ni mambo yanayochochea mshikamano, heshima na ushirikiano kazini,” amesema Dkt. Mwakujonga.
Kwa upande wake, Afisa Tawala wa Idara ya Huduma za Kitawala, Bi. Clara Paschal Kille, amesema kuwa bonanza hilo limechangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza afya za wafanyakazi kupitia michezo mbalimbali, huku akisisitiza umuhimu wa michezo ya akili kama draft, bao na karata katika kuimarisha uwezo wa kufikiri na kupunguza msongo wa mawazo.
“Ni muhimu kwa wafanyakazi kushiriki matukio kama haya mara kwa mara kwa sababu yanatoa nafasi ya pekee ya kubadilishana mawazo nje ya mazingira ya ofisi,” amesema Bi. Kille.
Bi. Kille ametoa wito kwa wafanyakazi wote wa Ndaki hiyo kuhakikisha wanajitokeza kuchangamkia fursa ya kushiriki bonana kwani ni muhimu kwao.
Naye Naibu Mshauri wa Wanafunzi wa Ndaki hiyo, Bi. Zitta Victoria Mnyanyi, amesema kuwa kila mwaka chuo hutenga siku maalum kwa ajili ya wafanyakazi kukutana, kuburudika na kujifunza kutoka kwa wenzao katika mazingira tofauti na eneo la kazi.
Amesisitiza umuhimu wa kushiriki michezo ili kuwa afya njema, mshikamano na maelewano kwani ni msingi wa utendaji kazi wenye mafanikio kwa Taifa.
“Tukio hilo limeonyesha dhahiri kuwa ushirikiano ni msingi wa mafanikio, Wafanyakazi wenye afya njema na maelewano hutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi,” amesema Mnyanyi.
Wafanyakazi walioshiriki katika bonanza hilo walionekana kufurahia kila tukio, huku wakieleza kuwa michezo hiyo imewasaidia kujifunza, kupumzika na kufungua akili kwa namna mpya, huku wakipongeza uongozi wa Ndaki kwa kuwawezesha kushiriki bonanza hilo na kuahidi kuwa mabalozi wa mshikamano kazini.
Chuo Kikuu Mzumbe ni miongoni mwa taasisi bora za elimu ya juu nchini, na kujivunia kutoa elimu bora yenye kulenga maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla, kwa mujibu wa kauli mbiu yao “Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu.”