Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Ushirika Kinjolu kata ya Kikolo Halmashauri ya Mji Mbinga Mkoani Ruvuma Bosco Turuka kushoto,akikagua uzalishaji wa Kahawa katika moja la shamba la mkulima katika kijiji cha Kikolo jana,wengine Pichani ni baadhi ya Wanachama wa Chama wa Kinjolu Amcos.
………
Na Mwandishi Wetu, Mbinga
WAKULIMA wa Kahawa wanaohudumiwa na Chama cha Msingi cha Ushirika KINJOLU AMCOS kata ya Kikolo na Kihungu Halmashauri ya Mji Mbinga Mkoani Ruvuma,wameiomba Serikali kukomesha vitendo vya wafanyabiashara wanaonunua kahawa kwa magendo na wengine kununua kahawa ikiwa bado shambani.
Mwenyekiti wa Chama hicho Bosco Turuka alisema,wafanyabiashara wanapita mashambani kila msimu wa mavuno na kuwarubuni wakulima wauze kahawa kwa bei ndogo kwa kutumia vipimo haramu vya magoma vinavyowanyonya na kuwarudisha nyuma kiuchumi wakulima.
Alisema,iwapo Serikali itafanikiwa kukomesha vitendo hivyo wakulima watapata fedha nyingi na kuongeza uzalishaji hasa baada ya Serikali ya awamu ya sita kuanzisha mpango wa kutoa mbolea za ruzuku kwa wakulima wa zao hilo.
Kwa mujibu wa Turuka,mpango wa mbolea za ruzuku umeongezeka uzalishaji wa kahawa kutoka tani 93 msimu wa kilimo 2022/2023 hadi kufikia tani 192 msimu wa mwaka 2024/2025.
Aidha alisema,mbolea za ruzuku zimewezesha kuongezeka kipato kuboresha maisha ya wanachama na wakulima kwa kujenga nyumba bora,kununua vyombo vya usafiri,kusomomesha watoto na kuhamasisha wakulima wengi kujiunga na Ushirika kutoka wanachama 93 hadi 300.
Alisema,kutokana na usimamizi wa Serikali kupitia mfumo wa stakabadhi gharani msimu wa 2024/2025 wakulima wameuza kahawa kwa bei nzuri tofauti na makampuni au watu binafsi wangeruhusiwa kununua kahawa basi wakulima wasingepata fedha nyingi.
Turuka,ameiomba Serikali kufanya matengenezo ya barabara ili kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji wa mazao kutoka shambani na kupeleka sokoni kwani ubovu wa barabara unatoa nafasi kwa wafanyabiashara kwenda moja kwa moja mashambani kununua mazao kwa bei ndogo.
Mkulima Gotan Komba,ameipongeza Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan,kufufua na kuimarisha sekta ya ushirika kwani imewezesha kulima kwa tija na kuongeza uzalishaji wa kahawa na mazao mengine mashambani.
Alisema,kwa muda mrefu walikuwa wanalima lakini hawakupata manufaa makubwa kutokana na gharama kubwa za uzalishaji lakini baada ya Serikali kuanza mpango wa kutoa mbolea za ruzuku umesaidia sana kupungunza gharama za uzalishaji wa kahawa na kuongeza ukubwa wa mashamba yao.
Komba,ameiomba Serikali kuendeleza mpango huo kwa kutoa pembejeo hasa mbolea na dawa za kuuwa wadudu kwani umesaidia sana kuhamasisha wananchi wengi kujikita kwenye kilimo cha zao la kahawa ambalo ni uti wa mgongo katika Wilaya ya Mbinga na Mkoa wa Ruvuma.
Mkulima mwingine wa kijiji cha Kikolo Hilda Komba,amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango na juhudi za wakulima wa kahawa hasa baada ya kutoa ruzuku kwenye mbolea ambazo zimechangia sana uzalishaji wa zao hilo.
Ameipongeza Wizara ya kilimo kwa kutoa bure miche bora ya kahawa kwa wakulima ambayo inakwenda kuongeza uzalishaji na kuboresha maisha ya wakulima,kuchochea kukua kwa uchumi wa Wilaya ya Mbinga,Mkoa wa Ruvuma na Taifa.