Na. WAF, Tabora
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ameiasa jamii kuwa mstari wa mbele kuhakikisha watoto wote wanaostahili kupata chanjo wanapata ili kujikinga na magonjwa kwakuwa mtoto asipopata chanjo anakuwa hatarini kupata maambukizi ya magonjwa.
Waziri Mhagama ameyasema hayo leo Aprili 28, 2025 Mkoani Tabora wakati akizindua Maadhimisho ya Wiki ya Chanjo Kitaifa yanayoenda sambamba na kauli mbiu isemayo “Chanjo ni Kinga; Tuungane kuwezesha Walengwa wote watape Chanjo.”
Amesisitiza jamii kuendelea kutumia wiki ya chanjo kama fursa ya kuhakikisha walengwa na watoto wote wanapata chanjo kulingana na ratiba na kuvielekeza vituo vya kutolea huduma za chanjo kuendelee kuwahudumia wananchi wote wanaohitaji huduma za Afya hususan huduma za chanjo.
“Maadhimisho haya yatafanyika sambamba na utoaji wa chanjo zote ikiwemo chanjo ya kukinga saratani ya mlango wa kizazi kwa mabinti wenye umri wa miaka tisa (9) ambayo itamsaidia kumkinga dhidi ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi hivyo kwa wale mabinti ambao hawakupatiwa chanjo ni vema wapatiwe ili kuwakinga,” amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama ameeleza kuwa takwimu za hivi karibuni zinaonesha kwa miaka mitano (5) mfululizo kiwango cha uchanjaji kitaifa ni zaidi ya asilimia 90 na hivyo kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika utoaji wa huduma za chanjo.
“Kiwango hiki cha uchanjaji hapa nchini, pamoja na afua nyingine, imewezesha nchi kufikia malengo ya Milenia (SDG 4) kwa kupunguza vifo vya watoto chini ya umri miaka mitano,” amesema Waziri Mhagama.
Waziri Mhagama amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na Shirika la utoaji wa Chanjo Duniani (GAVI) ina mikakati mingi ya kuhakikisha huduma za afya hususani chanjo zinaendelea kuboreshwa ambapo imeweza kuimarisha mnyororo baridi wa utunzaji wa chanjo katika vituo vya kutolea huduma za afya hapa nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa huduma za uuguzi na Ukunga Wizara ya Afya Bi. Ziada Sellah akimuwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema dhima ya maadhimisho hayo ni kuwaleta wadau pamoja na wataalam ili kujadili namna bora ya kuendelea kutoa huduma bora za chanjo katika mkoa wa Tabora na nchi nzima kwa ujumla.
“Madhumuni mengine ya maadhimisho haya ni kuhamasisha na kuelimisha jamii umuhimu wa huduma za chanjo katika kukinga magonjwa ambayo yanaweza kuzuilika kwa chanjo ikiwemo, Surua Rubella, Nimonia pamoja na chanjo ya kuzuia kuhara,” amesema Bi. Ziada
Mwakilishi Mkazi Shirika la Afya Duniani Tanzania (WHO) Dkt. Charles Sagoe-Moses amesema uchaguzi wa mkoa wa Tabora kuwa mkoa wa uzinduzi wa kitaifa kwa mwaka huu ni wa kupongezwa kutokana na baadhi ya watoto walio wengi ambao ni walengwa wa chanjo kutofikiwa.
“WHO imeendelea kuunga mkono katika kushughulikia pengo hilo kwa kutoa msaada wa chanjo ambayo ililenga wilaya tatu (3) za Kaliua, Sikonge na Uyui, zilizotajwa kuwa na idadi kubwa ya dozi sifuri, kampeni ililenga kufikia vijiji vyote na ilikuwa na mafanikio makubwa ” amesema Dkt. Charles.