Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb), akizungumza katika Jukwaa la Ufadhili wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2025 (ECOSOC Forum on Financing for Development Follow-Up (FfD Forum), lililowahusisha mawaziri wa Fedha, Mipango, Mambo ya Nje na sekta nyingine pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo yakiwemo mashirika ya Fedha ya Kimataifa kwa ajili ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa Maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo, lililofanyika Makao Makuu ya Umoja huo, Jijini New York, nchini Marekani.

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb) (Kulia) akipigwa picha (Selfie) ya kumbukumbu na Mshauri wa Masuala ya Uchumi na Kijamii wa Serikali ya Marekani, Bi. Mariya Ilyas, wakati wa Jukwaa la Ufadhili wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2025 (ECOSOC Forum on Financing for Development Follow-Up (FfD Forum), lililowahusisha mawaziri wa Fedha, Mipango, Mambo ya Nje na sekta nyingine pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo yakiwemo mashirika ya Fedha ya Kimataifa kwa ajili ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa Maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo, lililofanyika Makao Makuu ya Umoja huo, Jijini New York, nchini Marekani.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, New York, Marekani)
….
Na Benny Mwaipaja, NewYork
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ametoa rai kwa nchi zilizoendelea kupunguza gharama za mikopo na kutoa muda mrefu wa kulipa madeni ili kuziwezesha nchi zinazoendelea zikiwemo za Afrika kutekeleza miradi ya maendeleo itakayochochea ukuaji wa uchumi na maisha ya wananchi kwa ujumla.
Mhe. Dkt. Nchemba ametoa rai hiyo jijini NewYork nchini Marekani, wakati akichangia mada katika Jukwaa la Ufadhili wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2025 (ECOSOC Forum on Financing for Development Follow-Up (FfD Forum), linalofanyika Makao Makuu ya Umoja huo, Jijini NewYork nchini humo.
Alisema kuwa Mbinu za utoaji wa viwango vya mikopo zinapaswa kubadilika ili kuakisi kwa usahihi uwezo wa kweli wa nchi zinazoendelea kulipa madeni na kuhimiza matumizi zaidi ya fedha mchanganyiko (blended finance), upanuzi wa dhamana za hatari kutoka kwa Benki za Maendeleo ya Kielelezo (MDBs), na utekelezaji wa mipango ya uwazi wa madeni ili kusaidia kupunguza gharama za hatari zinazoonekana.
Dkt. Nchemba alipongeza juhudi zinazofanywa na mataifa pamoja na taasisi za fedha zinazokopesha kwa kuboresha upatikanaji wa mikopo nafuu lakini kwa nchi nyingi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania, inakwazwa na viwango vikubwa vya gharama za mikopo na ulipaji wa madeni husika unaoathiri bajeti za nchi hizo.
Alipendekeza masuala matatu ya kufanyiwa kazi ikiwemo upatikanaji wa mikopo nafuu, kuongeza kasi ya kurekebisha muundo wa ulipaji madeni, kuwezesha upatikanaji wa mikopo mchanganyiko (blended finance) inayozingatia mahitaji pamoja na kuzisaidia nchi zinazoendelea kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Akizungumzia umuhimu wa sekta binafsi katika kukuza uchumi, Dkt. Nchemba alisema kuwa uwekezaji wa sekta binafsi ni muhimu ili kutimiza malengo ya maendeleo ya milenia kwa kujenga uchumi himilivu, jumuishi na kuhakikisha hakuna mtu anayeachwa nyuma kimaendeleo.
Alishauri kuimarisha majukwaa ya kuwezesha uwekezaji ambayo yanaunganisha fursa na mitaji ya kimataifa, kuchochea athari chanya, na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma na kwamba Tanzania iko tayari kushirikiana na washirika wote kufungua uwekezaji binafsi kwa maendeleo jumuishi na endelevu.
Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania, chini ya uongozi mahili wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imefanya mageuzi makubwa ya kisera ya upatikanaji wa fedha, kuweka uwazi wa matumizi na kutanua wigo wa upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum.
“Tunaendeleza ujumuishaji wa kifedha kupitia majukwaa ya kidijitali na kufanikisha urasimishaji wa sekta isiyo rasmi ili kuongeza upatikanaji wa masoko na fedha. Kwa ngazi ya kimataifa, tunatoa wito wa kuoanisha kwa kiwango kikubwa zaidi uwekezaji binafsi na vipaumbele vya kitaifa, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, na kuanzisha taasisi za msaada kama Kituo cha Kimataifa cha Msaada wa Uwekezaji kwa Nchi Zenye Maendeleo Duni (LDCs)” alisema Dkt. Nchemba.
Alisema kuwa Kitaifa, Tanzania inatengeneza mikakati ya fedha endelevu, dhamana zenye mwelekeo mahsusi (thematic bonds), na inatumia ubunifu wa kidijitali ili kuvutia rasilimali. kuanzisha mifumo ya uwekezaji kutoka kwa diaspora na kuhamasisha uwekezaji katika miundombinu endelevu na inayostahimili mabadiliko ya tabianchi.
Alishauri kuimarisha majukwaa ya kuwezesha uwekezaji ambayo yanaunganisha fursa na mitaji ya kimataifa, kuchochea athari chanya, na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma na kwamba Tanzania iko tayari kushirikiana na washirika wote kufungua uwekezaji binafsi kwa maendeleo jumuishi na endelevu.
Jukwaa la Ufadhili wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa linawahusisha mawaziri wa Fedha, Mipango, Mambo ya Nje na sekta nyingine pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo yakiwemo mashirika ya Fedha ya Kimataifa kwa ajili ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa Maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo.