Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akijibu maswali bungeni wakati wa Kikao cha 15 Mkutano wa 19 wa Bunge jijini Dodoma leo tarehe 30 Aprili, 2025.
……………..
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inatarajia kutekeleza Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya tabianchi katika jamii za Wazanzibari zilizoathiriwa na maji chumvi na kukosa maji baridi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis bungeni jijini Dodoma leo tarehe 30 Aprili, 2025 wakati akijibu swali la Mbunge wa Gando Mhe. Mussa Omar Salim aliyetaka kujua ni lini ahadi ya Serikali ya kuzuia maji chumvi kuingia katika Bonde la Mpanja- Gando itatekelezwa.
Akiendelea kujibu swali hilo, Naibu Waziri Khamis amesema Ofisi hiyo kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imeandaa maandiko manne ya miradi yenye thamani ya Dola za Marekani milioni 10.
Naibu Waziri Khamis ameongeza kwa kusema kuwa maandiko yaliyoandaliwa, tayari yamewasilishwa kwenye Mfuko wa Kimataifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi (Adaptation Fund) na Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya hatua zaidi.
Ameendelea kueleza kuwa shughuli za kuzuia maji chumvi katika Bonde la Mpanja Gando zitaanza kutekelezwa baada ya fedha kupatikana kupitia miradi hiyo ili wananchi wa maeneo hayo waweze kuendelea na shughuli zao.
Katika swali la nyongeza kuhusu iwapo katika maandiko hayo Serikali inaweza kutoa kipaumbele na kuweka bajeti katika Jimbo la Gando ili kuwalinda wananchi na mashamba yaliyoathiriwa kwa kujaa maji.
“Tulifika Gando na Mheshimiwa Dkt. Kijaji (aliyekuwa Waziri) tukaona maji yameingia kwenye makazi ya watu na mashamba, namuomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwa na subira tunafanya taratibu na zitakapopatikana fedha tunakwenda kuondosha tatizo hilo pia katika maeneo mengine yakiwemo Nungwi, Lindi na Mtwara, na nimwambie Jimbo la Gando tutalipa priority (kipaumbele) kwasababu ya changamoto ambayo tumeiona pale,” amefafanua Mhe. Khamis.
Hivyo, kwa kuwa miradi fedha za utekelezaji wa miradi hiyo bado hazipatikana kutoka kwenye Mfuko huo kutokana na kumalizika kwa muda wa ithibati ya NEMC kwenye Mfuko huo.
Naibu Waziri Khamis amesema mchakato wa kuhuisha ithibati hiyo unaendelea hivyo utekelezaji wa miradi utaanza baada ya NEMC kupata ithibati na miradi hiyo kufanyiwa mapitio kwa ajili ya upatikanaji wa fedha hizo.
Itakumbukwa Mfuko wa Kimataifa wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi imekuwa ikitoa fedha kwa ajili ya kufadhili miradi mbalimbali ya hifadhi ya mazingira katika maene mbalimbali nchini Tanzania.