WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mhe. Shariff Ali Shariff ametoa wito kwa wananchi na wafanyakazi wote kushiriki kikamilifu katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, yatakayofanyika tarehe 1 Mei 2025 kisiwani Pemba.
Akizungumza na waandishi wa habari kuelekea maadhimisho hayo, Waziri Shariff alieleza kuwa siku hiyo ni muhimu katika kuenzi mchango wa wafanyakazi katika maendeleo ya taifa. “Tunapokaribia siku ya Mei Mosi, ni wakati wa kutafakari umuhimu wetu kama wafanyakazi na nguvu yetu tunayoitumia kujenga taifa letu,” amesema.
Ameeleza kuwa mwaka huu, Serikali imeandaa ratiba maalum ya kuadhimisha siku hiyo katika mikoa yote ya Unguja na Pemba, ili kutoa fursa kwa wananchi kushiriki kwa pamoja.
Katika kuhamasisha ushiriki mpana wa jamii, Waziri ametoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi bila kukosa. “Shime tushiriki kwa wingi bila kukosa, ni wakati wa kuonyesha mshikamano wetu na kuthamini mchango wa kila mfanyakazi,” amesisitiza.
Ameeleza kuwa katika kuelekea kilele cha maadhimisho hayo, shughuli mbalimbali zimepangwa kufanyika ikiwemo semina, usafi wa mazingira, michezo, makongamano na burudani kwa wafanyakazi na wananchi.
Aidha amesema kutakuwa na maonesho ya kazi za mikono na huduma kutoka taasisi mbalimbali, sambamba na maandamano ya amani ya wafanyakazi yatakayopokelewa rasmi na viongozi wa serikali.
Waziri Shariff alitoa hakikisho kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kulinda raia na kuhakikisha maadhimisho yanafanyika katika hali ya amani na utulivu. “Vyombo vyetu vya ulinzi viko tayari kuhakikisha kila mmoja anashiriki kwa usalama,” almesema.
Pia ametoa shukrani kwa wafanyakazi wastaafu na wale waliopo kwa mchango wao mkubwa kwa taifa na kusisitiza kuwa serikali itaendelea kutambua na kuthamini jitihada zao katika kukuza uchumi na maendeleo ya kijamii.
Kwa upande mwingine, Waziri aliwaomba wananchi kufuata taratibu zitakazotolewa na mamlaka husika kuhusu usafiri na ratiba ya shughuli, huku akiahidi kuwa taarifa rasmi zitatolewa mapema ili kila mmoja aweze kushiriki.
Katika Maadhimisho hayo ambayo Mgeni Rasmi ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi yatafanyika Kizimkazi Mkoa wa Kusini Kwa Unguja na Kwa Pemba yataadhumishwa Wawi huku Kauli mbiu ni “Wafanyakazi tufanye kazi kwa bidii na nidhamu, tudai haki zetu kwa mujibu wa Sheria na tushirikiane katika Uchaguzi Mkuu kwa Amani.” Kaulimbiu hii inalenga kuhimiza uwajibikaji kazini na mshikamano kuelekea Uchaguzi Mkuu.