Na Mwandishi wetu, NCAA.
Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) imeendesha mafunzo maalum kwa watumishi wake, yakilenga kuboresha utendaji kazi kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma pamoja na kuimarisha mshikamano na uwajibikaji kazini.
Mafunzo hayo yaliyofanyika Aprili 30, 2025 katika ofisi za Makao Makuu ya NCAA, Karatu yalijikita katika kuwajengea watumishi msingi wa kimaadili ili kuongeza tija katika utendaji wao wa kila siku.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Mariam Kobelo alisema kuwa mafunzo kwa watumishi ni sehemu ya mkakati wa NCAA kuendeleza rasilimali watu ndani ya taasisi.
Kobelo alisisitiza kuwa mbali na kuongeza weledi, mafunzo hayo yanasaidia kujenga mshikamano kazini na kuwawezesha watumishi kujiimarisha kimaadili, nidhamu na uwajibikaji sehemu za kazi.
Mafunzo hayo yalitolewa na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali za Serikali zikiwemo Ofisi ya Rais – Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma (Kanda ya Kaskazini), Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Karatu, na Chuo Kikuu cha Mzumbe.
Mada zilizotolewa ni pamoja na maadili ya utumishi wa umma, Utunzaji wa Muda na Ushirikiano kazini, Rushwa mahala pa kazi, utunzaji wa kumbukumbu katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Aidha, kwa upande wa Watumishi mafunzo hayo yamewapa ari mpya ya kujitathmini binafsi kwa kuzingatia maadili ya kazi, huku wakisisitiza kuwa wataendelea kuwa mabalozi wa maadili kazini kwa kuhamasishana na kushirikiana kwa karibu katika kutimiza malengo ya shirika.