Na Silivia Amandius
Bukoba, Kagera.
Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeandika historia mpya katika Tarafa ya Katerero, mkoani Kagera, kwa kukamilisha ujenzi wa bweni la kisasa kwa ajili ya watoto wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Lyamahoro A, iliyopo Kata ya Nyakibimbili.
Mradi huu unaogharimu shilingi milioni 128, umelenga kutoa makazi salama na huduma bora kwa takriban wanafunzi 80, ambao hapo awali walilazimika kutembea umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni, hali iliyokuwa hatarishi na ya kuchosha kwa watoto hao.
Tarafa ya Katerero, inayojumuisha kata kama Nyakibimbili, Ibwera na Kaibanja, ina idadi kubwa ya watoto wenye ulemavu na mahitaji maalum. Kukosekana kwa bweni la kuwahudumia ilikuwa moja ya changamoto kubwa iliyowafanya wengi kushindwa kuhudhuria shule au kuacha kabisa masomo.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa bweni hilo lililokamilika, Afisa Tarafa Bwanku M. Bwanku, akiwa na viongozi wengine wa kijiji, alisema hatua iliyofikiwa ni ya kujivunia, huku akiahidi kusimamia ukamilishaji wa miundombinu ya maji, umeme na ununuzi wa vitanda ili wanafunzi waanze kulitumia haraka iwezekanavyo.
“Zamani miradi ya namna hii ilikuwa ni ndoto kwa vijiji vya pembezoni, lakini chini ya uongozi wa Rais Samia, miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa usawa mijini na vijijini,” alisema Bwanku kwa furaha.
Mradi huu ni sehemu ya jitihada za Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kuhakikisha kuwa watoto wote, wakiwemo wenye mahitaji maalum, wanapata haki yao ya msingi ya elimu katika mazingira rafiki na salama.