WAFANYAKAZI kazi wa Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) wameungana na wafanyakazi wengine duniani kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Dunia na ahadi ya kuongeza juhudi katika utekelezaji wa majukumu yao ili kufikia malengo ya Kampuni.
Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika leo Mei 1, 2025 Jijini Dar es Salaam, Meneja Rasilimali Watu wa ETDCO, Bi. Grance Sondi, amesema kuwa uongozi wa Kampuni umejipanga kuweka mikakati rafiki inayolenga kuongeza hamasa kwa wafanyakazi, hasa katika masuala ya ushirikiano kazini ili kuleta tija kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
“ETDCO itaendelea kuimarisha mazingira bora ya kazi na kuhamasisha mshikamano miongoni mwa wafanyakazi, jambo ambalo litachochea ufanisi katika utekelezaji wa Miradi ya Umeme nchini,” amesema Sondi.
Aidha, amewataka Wafanyakazi kuongeza bidii na kuwajibika kikamilifu katika kutimiza majukumu yao ya kila siku ili kusaidia kufikia lengo la kutoa huduma bora ya umeme wa uhakika kwa wananchi
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TUICO Tawi la ETDCO, Bi. Monica Lymo, ameeleza kufurahishwa na ushiriki wa kampuni katika maadhimisho hayo, huku akibainisha kuwa ni ishara ya kuthamini mchango wa wafanyakazi.
“Leo tunajivunia mshikamano, ushirikiano na upendo tuliojengewa na uongozi wa ETDCO. Hii imetuwezesha kutekeleza Miradi kwa wakati na kwa mafanikio makubwa,” amesema Lymo.
Ameongeza kuwa kuwa wafanyakazi wa ETDCO wamejipanga kuendelea kuwa mfano kwa Taasisi nyingine nchini kwa kuwa na utendaji kazi unaolenga matokeo chanya.
Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kauli mbiu isemayo: “Uchaguzi Mkuu 2025 Utaleta Viongozi Wanaojali Haki na Maslahi ya Wafanyakazi, Sote Tushiriki.” Mgeni rasmi katika tukio hilo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila.