Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Urambo mkoani Tabora leo Mei 2, 2025, wakati wa ziara ya kukagua Mradi wa Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza Umeme wa Msongo wa Kilovolti 132/33 kilichopo eneo la Uhuru, Wilayani Urambo. Mradi huo umetekelezwa na Kampuni ya ETDCO.
……
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, ameipongeza Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO) chini ya uongozi wa Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni hiyo CPA. Sadock Mugendi kwa kutekeleza kwa ufanisi mradi wa ujenzi wa laini ya kusafirisha umeme ya kilovolti 132 kutoka Tabora hadi Urambo.
Akizungumza leo Mei 2, 2025, Mkoani Tabora wakati wa ziara ya kukagua Mradi wa Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza Umeme cha Msongo wa Kilovolti 132/33 kilichopo eneo la Uhuru, Wilayani Urambo, Dkt. Biteko, amesema kuwa ETDCO imefanya kazi kubwa ya kuhakikisha wanatekeleza mradi kwa wakati na kuleta tija kwa Taifa.
Dkt. Biteko amesema kuwa kutokana na utendaji mzuri wa ETDCO, wana haki ya kupewa miradi mingine ya aina hii kwa kuwa wameonyesha uwezo mkubwa wa utekelezaji.
“Tangu kituo hiki kianze kufanya kazi, mapato ya TANESCO yameongezeka kwa asilimia 10 ndani ya siku 20 tu. Hii inaonyesha namna mradi huu ulivyokuwa muhimu kwa wananchi na Taifa kwa ujumla,” amesema Dkt. Biteko.
Amesema kuwa mwaka jana alipokuja katika mradi huo ulikuwa umefikia asilimia 10, huku akieleza kuwa mpaka sasa mradi umemalika kabla ya muda. “Hongereni sana, endeleeni kufanya kazi – kazi itawatetea popote pale,”
Dkt. Biteko amesema kuwa Serikali imewekeza jumla ya shilingi bilioni 44 katika mradi huo; ambapo bilioni 24 zilitumika kwa ujenzi wa laini ya umeme kutoka Tabora hadi Urambo, bilioni 16 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme na bilioni 4 kulipa fidia kwa wananchi waliopisha mradi.
Amesema kuwa kabla ya mradi huu, Wilaya ya Urambo ilikuwa inakusanya wastani wa shilingi milioni 327 kwa mwezi, lakini sasa mapato hayo yameongezeka kwa asilimia 10, na TANESCO inatarajia kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 4.5 kwa mwaka katika wilaya hiyo.
Kwa upande wake, CPA Mugendi ameahidi kuwa ETDCO itaendelea kutekeleza miradi yote kwa wakati, kwa ubora wa hali ya juu na kwa gharama nafuu ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora ya umeme.
Wananchi wa Wilaya za Urambo na Kaliua wameishukuru serikali kwa kufanikisha mradi huo, wakisema umeme wa uhakika sasa umewapa nguvu ya kukuza shughuli zao za kiuchumi na kijamii.