Mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima, akiwasaidia wananchi kuhakiki majina yao kabla ya kwenda kuboresha taarifa zao katika Kituo cha kuandikisha wapiga kura, Ofisi ya Kata ya Isevya, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, wakati alipotembelea na kukagua vituo vya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili linalokwenda sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura Mkoani Tabora, leo Mei 04, 2025. Picha na INEC
Mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima, akimkabidhi kadi ya mpiga kura Mwanafunzi wa Kidato cha Sita wa Shule ya Sekondari ya Milambo, Maboto Wambura, wakati alipokitembelea Kituo cha Kuandikisha Wapiga Kura katika shule hiyo iliyopo Kata ya Chemchem, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mei 4, 2025. Picha na INEC
Mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima, akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana Tabora, wakati alipotembelea Kituo cha Kujiandikisha Wapiga Kura kilichopo shuleni humo, Mei 04, 2025, ambapo pia aliwahamasisha wanafunzi wa shule hiyo na Sekondari ya Milambo zilizopo katika Hamlashauri ya Manispaa ya Tabora, wajitokeze kujiandikikisha kwa walio na sifa. Picha na INEC.
Mkurugenzi wa Tume Huru ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima (kulia), akizungumza na mwendesha kifaa cha ‘Bayometriki’ katika Kituo cha kuandikisha wapiga kura kilichopo Kata ya Isevya, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, alipotembelea na kukagua vituo vya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili linalokwenda sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura Mkoani Tabora, leo Mei 04, 2025. Katikati ni Mratibu wa Uandikishaji Mkoa wa Tabora, Elihuruma Nyella. Picha na INEC
…………….
Na Mwandishi Wetu, Tabora.
MKURUGENZI wa Tume Huru ya Uchaguzi, Ramadhani Kailima amewataka wananchi wa Mkoa wa Tabora kujitokeza kuhakiki na kuboresha taarifa zao katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura kwenye vituo walivyojiandikishia na kutazama daftari la awali lilolowekwa wazi na kutoa taarifa za wale waliokosa sifa kuwepo kwenye daftari hilo
Kailima amezungumza hayo Mei 4, 2025 wakati alipokuwa anatembelea na kukagua vituo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ambapo amesema wananchi wameonesha mwitikio mkubwa kwa kujitokeza kuhakiki taarifa zao.
Alisema Tume imeweka wazi daftari la awali la wapiga kura katika vituo vyote vilivyotumika kuandikisha na kuboresha taarifa za wapiga kura katika awamu ya pili hivyo wananchi wajitokeze kuhakiki taarifa zao na kutoa taarifa za wale ambao hawastahili kuwepo katika Daftari hilo.
“Wananchi endapo wataona katika Daftari ambalo tumeliweka katika kila kituo kuna mwananchi ambaye amekosa sifa kama vile kufariki basi wawe huru kwa kutumia fomu namba 5B kumuondoa huyo ambaye amekosa sifa za kuwepo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” alisema Kailima.
Aliongeza kuwa, Mkoa wa Tabora unavituo vya kujiandikishia daftari la mpiga kura vipo 376 mkoa mzima. Hata hivyo, alisisitiza wananchi waendelee kujitokeza katika kuboresha taarifa zao wale ambao hawakuboresha taarifa zao katika awamu ya kwanza ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura basi ndio kipindi cha kafanya hivyo.
Aidha, tume inatoa nafasi kwa watu wote wenye changamoto ya kutoa kuona kusikia na kutoajua kusoma wanatakiwa kuja na watu wao wenye uwezo wa kuwasaidia ili waeze kujiandikasha kwenye Daftari la mpiga kura .
Kwa upande wake, Mratibu wa Uandikishaji Mkoa wa Tabora, Elihuruma Nyella alisema hali ya uandishikishaji katika Mkoa wa Tabora unaendelea vizuri na watu wanajitokea.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili unafanyika sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura kuanzia Mei 01, 2025 na kukamilika tarehe 07, 2025 katika mikoa 15 ya mzunguko wa kwanza katika awamu ya pili ya uboreshaji.