Wanasayansi wa mazingira wametakiwa kutumia lugha rahisi zinazoweza kueleweka na jamii katika kuwasilisha tafiti zao hatua ambayo kwa namna moja ama nyingine itasaidia kuwepo kwa uhifadh jumuishi na endelevu.
Mbali na lugha rahisi pia wanasayansi hao wa mazingira wametakiwa kutumia njia mbalimbali na rahisi ikiwepo hadithi kuwasilisha tafiti zao kwa jamii.
Wito huo umetolewa leo Mei 3, 2025 kwenye mafunzo kwa wanasayansi wa mazingira juu ya namna bora ya kuwasilisha tafiti zao mafunzo yaliyoandaliwa na Shirika la Grumeti Fund kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Leiden (Uholanzi).
Akitoa mada katika mafunzo hayo, Mwenzeshaji Ghaamid Abdulbasat amesema upo umuhimu mkubwa wa mawasiliano ya sayansi katika kushawishi sera na ufahamu wa umma na kwamba ili umma uweze kuelewa na kushiriki kikamilifu ni lazima lugha inayotumika iweleke vema kwao.
“Kwa miaka mingi wanasayansi wamewasiliana baina yao pekee hivyo kusababisha ujumbe husika kubaki miongoni mwao kwahiyo ili kuleta mabadiliko, lazima tuzungumze kwa njia ambazo umma unaweza kuhusiana nao.” amesema
Amesema ili kuleta mabadiliko chanya katika suala zima la uhifadhi endelevu ni lazima wanasayansi hao wahakikishe wanatumia mbinu mbalimbali kufikisha ujumbe kwa jamii ili jamii iweze kuelewa na kushiriki kikamilifu katika kutekeleza yale yaliyobainishwa kupitia tafiti hizo.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayom wanafunzi wa shahada ya uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam ,Janeth Mgure amesema wasomi wengi wamekuwa na tabia ya kutumia lugha ngumu bila kujali kama ujumbe ubadika kwa walengwa.
“Kwa wasomi wengi lugha tunayotumia mara nyingi ni ngumu kwa jamii kuelewa tumejisahau kuwa jamii hii ni wadau muhimu katika kufanikisha kile tulichokusudia kupitia mafunzo haya nimeona ipo haja ya sisi kubadilika,” amesema
Mgure ambaye pia ni mwanzilishi mwenza wa Shirika la Human – Wildlife Co-exsistance Foundation amesema mafunzo waliyopata yamewapa uelewa mkubwa hivyo yatatumika kuziba pengo la mawasiliano lilikuwepo kati yao na jamii.
Awali akieleza lengo la mafunzo hayo, Mratibu wa Programu ya Utafiti na Ubunifu (RISE) kutoka Grumeti fund Victoria Mkesa amesema mafunzo hayo yameandaliwa kwa wanasayansi hao ili kusaidia kuimarisha uwezo wao wa kuwasiliana na jamii kupitia hadhiti na lugha rahisi.
Amesema mafunzo hayo yaliyoshirikisha wanasayansi wa mazingira 10 kutoka taaisisi mbalimbali nchini yamefanyika kwa muda wa siku tano ambapo pia yamelemga kuwapa washiriki ujuzi na zana za kurahisisha lugha ya kisayansi na kushirikisha jamii kwa ufanisi zaidi kupitia hadithi zenye kueleweka kirahisi.
Amesema mafunzo hayo yamesisitiza juu ya hadithi kama zana yenye nguvu kuhimiza uhifadhi haswa nchini Tanzania ambapo masuala ya mazingira yanahusishwa sana na ardhi, historia na maisha.
Amesema wanasayansi kuwasilisha tafiti zao kwa njia zinazoweza kueleweka na zinazozingatia wanadamu kutasaidia uhifadhi jumuishi na endelevu na inatengeneza njia ya uhusiano mkubwa kati ya utafiti na uhalisia ambapo uhifadhi hauko kwenye vitabu tu, bali wenye kusikika, kueleweka na kutendewa kazi.