Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza Protas Henry akitoa taarifa kwa wandashi wa habari (hawapo pichani)
Na Hellen Mtereko,Mwanza
Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza kwakushirikiana na wadau wa kamati ya uhakiki ya Wilaya ya Nyamagana wameokoa kiasi cha shilingi milioni 700 kwenye mikopo ya vikundi inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa mwaka 2024/2025.
Hayo yamebainishwa Leo Alhamis Mei 08, 2025 na Kaimu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mwanza Protas Henry wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari.
Alisema fedha hizo ziliokolewa kutokana na uhakiki na udhibiti uliofanyika kwenye utoaji wa mikopo ya vikundi vya wanawake,vijana na watu wenye ulemavu.
“Katika uhakiki huo vikundi 41 havikukidhi vigezo na vilibainika na makosa mbalimbali yakiwemo ya kuomba mikopo kwa miradi hewa,kuwasilisha bei za juu za vifaa kuliko bei ya soko,kutokuwa na maeneo ya kufanyia biashara pamoja na kuomba mikopo kwaajili ya mradi wa mtu binafsi au familia”, alisema Henry
Ameongeza kuwa TAKUKURU imechukua hatua ya kufanya udhibiti wa kuziba mianya ya rushwa iliyojitokeza ili kusaidia Halmashauri kutoa mikopo kwa vikundi vilivyokidhi vigezo ambapo vikundi 87 vilikidhi vigezo kati ya 128 vilivyoomba mikopo na jumla ya bilioni 1.3 imeidhinishwa itolewe kwaajili ya vikundi hivyo.