Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 Ismail Ussi,akiangalia kahawa iliyosindikwa na Kiwanda cha kukoboa Kahawa Mbinga Mkoani Ruvuma(MCCCO)alipotembelea Banda la Kiwanda hicho wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Wilayani Mbinga jana,kushoto ni Afisa Mauzo wa MCCCO Edes Mapunda.
Afisa Mauzo wa Kiwanda cha Kukoboa Kahawa cha Mbinga Coffee Curing Company(MCCCO)kilichopo Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma Edes Mapunda akimuonyesha Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2025 Ismail Ussi baadhi ya bidhaa za kahawa zinazosindikwa katika Kiwanda hicho wakati wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Wilayani Mbinga jana.
Na Mwandishi Wetu, Mbinga
WANANCHI Mkoani Ruvuma,wametakiwa kuongeza kasi na mwamko wa kunywa kahawa ili kuboresha afya zao na kuimarisha soko la ndani la zao hilo kwa ajili ya kukuza uchumi wa Wakulima na Nchi kwa ujumla.
Wito huo umetolewa jana na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ussi, alipotembelea Banda la kiwanda cha kukoboa Kahawa cha Mbinga Coffee Curing Company(MCCCO)kwenye Uwanja wa Michezo wa CCM wakati wa mbio za Mwenge wa Uhuru Wilayani Mbinga.
Alisema,Wilaya ya Mbinga inazalishaji kahawa kwa wingi,yenye radha nzuri na ubora mkubwa,lakini Wananchi hawana utamaduni na utaratibu wa kunywa kahawa jambo linarudisha nyuma sekta ya kahawa hapa nchini.
Alisema,kahawa ni zao kubwa la kiuchumi na tegemezi kwa Wakulima wa Mbinga,Mkoa wa Ruvuma na Tanzania kwa ujumla,kwa hiyo kama Wananchi wataongeza kasi na utamaduni wa kunywa kahawa utaimarisha soko la ndani na kupunguza utegemezi kwenye soko la nje ambalo bei ikiyumba huathiri moja kwa moja pato na uchumi wa mkulima na Serikali.
Amewataka Wakulima,kuzingatia kanuni bora za uzalishaji wa kahawa na kusisitiza matumizi sahihi ya pembejeo na kutumia kiwanda chao cha MCCCO kuchakata kahawa ili kukidhi ubora,kuongeza thamani,bei ya zao hilo sokoni na kuepuka kuchakata kahawa majumbani.
Aidha amewasisitiza Wakulima Wilayani Mbinga,kuhakikisha wanapeleka kahawa yao katika kiwanda cha MCCCO kwa ajili ya kukoboa ili kiweze kufikia uwezo wake wa kukoboa tani 30,000 kwa mwaka.
“ili kiwanda kiweze kufanya kazi ni lazima Wakulima ambao ni sehemu ya wamiliki wahakikishe wanapeleka kahawa yao kwenye kiwanda cha MCCCO kwa ajili ya kukoboa badala ya kupeleka kwenye viwanda vingine,kinyume na hapo watarudisha nyuma malengo ya kiwanda chao”alisema Ussi.
Pia amewaasa Wakulima,kuongeza ukubwa wa mashamba ya kahawa na kuzalisha kwa wingi ili waweze kujiinua kimaisha kutokana na bei ya zao hilo kupanda kutoka Sh.4,500 mwaka 2023/2024 hadi Sh.9,000 mwaka 2024/2025.
Naye Afisa Mauzo wa MCCCO Edes Mapunda alisema,licha ya kiwanda hicho kutoa huduma bora na kwa wakati na uwezo wa kukoboa tani 30,000 kwa mwaka, lakini kinashindwa kufikisha uwezo wake kwani baadhi ya wakulima wanapeleka kahawa kwenye viwanda vya watu binafsi.
Alisema,kiwanda cha MCCCO kinamilikiwa kwa ubia kati ya Serikali na Wakulima kupitia Vyama vya Msingi vya Ushirika hivyo ni kiwanda cha wakulima wenyewe, wakipeleka kahawa kwenye kiwanda hicho watakuwa wanapeleke kwenye kiwanda chao.
Kwa mujibu wa Mapunda,hatua hiyo itasaidia sana kuongeza ajira kwa Wananchi wa Mbinga,Mkoa wa Ruvuma pamoja na kuongeza mapato ya Serikali yao.
“Wakulima wakileta kahawa kwenye kiwanda cha MCCCO kwa ajili ya kukoboa watakiwezesha kufikia uwezo wake na kutoa gawio kwenye Chama Kikuu cha Ushirika wa Kahawa(Mbifacu) kinachowakilisha Wakulima wa kahawa wa Wilaya ya Mbinga na Nyasa, faida zinazopatikana kupitia Mbifacu zinatoka katika kiwanda cha MCCCO”alisema Mapunda.
Mapunda,amewaomba Wakulima waendelee kuongeza uzalishaji mashambani ili kiwanda kiweze kufikisha malengo na kufanya hivyo watakijengea uwezo kiwanda chao badala ya kupeleka kwenye viwanda vya watu binafsi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mbinga Kelvin Mapunda alisema,katika msimu wa kilimo 2025/2026 Halmashauri imetoa miche zaidi ya 18,000 ya kahawa kwa Wakulima kama mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa katika Wilaya ya Mbinga.
Amewaomba Wananchi hususani wakulima,kupeleka kahawa kwenye kiwanda cha MCCCO kwa ajili ya kukoboa kwani faida inayopatikana kutoka kwenye kiwanda hicho inasaidia kuboresha huduma za kijamii ikiwemo pembejeo za ruzuku zinazotolewa kwa wakulima,afya na maji.