NORWAY
WAZIRI Mhandisi Masauni akiwa ameambatana na Ujumbe wa Tanzania pamoja na Balozi wa Norway Nchini Tanzania, amekutana na kufanya Mazungumzo na Bw. Bard Vegar Solhjell, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD) pamoja na Bi. Marita Sorheim Rensvik Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Maendeleo Endelevu katika Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Norwary.
Bi Marita aliambatana na timu ya wataalamu kutoka Idara ya Hali ya Hewa,wakala wa Mazingira na Taasisi ya Uchumi ya Bilojia (NIBIO).
Mazungumzo baina ya viongozi hao yalilenga kujenga na kuimarisha mahusiano ya kihistoria kati ya Tanzania na Norway kuhusiana na masuala ya mabadiliko ya Tabia Nchi, Mazingira pamoja na tafiti zinazofanyika kwa ufadhili wa shirika la NORAD.
Mazungumzo yalifanyika katika makao makuu ya shirika la NORAD jijini Oslo Norway.
Awali Mhandisi Masauni alizungumza na Bw. Solhjell, Mkurugenzi Mkuu wa NORAD na kuishukuru Serikali ya Norway, na taasisi yake ya NORAD kwa mchango wake mkubwa, katika kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya Tanzania. “Tanzania inathamini sana mchango mkubwa unaotolewa na NORAD katika Masuala ya kiufundi, kifedha, Utunzaji wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi; Uhifadhi wa misitu na utekelezaji wa mradi wa REDD+.
NORAD imechangia kwa kiasi kikubwa katika upatikanaji wa nishati mbadala na usambazaji wa umeme vijijini. Aidha ushirikiano wa NORAD umekuwa muhimu katika kuendeleza maisha ya jamii, ufahamu wa mazingira, na uwezo wa kitaasisi” amesema Mhe. Masauni.
Bwana Solhjell aliipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jitihada mbalimbali inazofanya ili kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi ikiwa ni pamoja na Kuanzisha Rasmi Kituo Cha Taifa Cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC ) ambacho kilianzishwa rasmi kwa mujibu wa sheria Februari, 2025.”Nimesikia kituo hiki ni cha mfano na cha Kwanza Barani Afrika”Amesema Solhjell.
Kupitia Mazungumzo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bi,Marita, Ujumbe wa Tanzania kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais ulipata fursa ya kusikiliza mawasilisho mbalimbali ya miradi ya Mazingira inayotekelezwa na Serikali ya Norway maeneo mbalimbali duniani ikiwa ni pamoja na nchini Tanzania. Mawasilisho hayo yalifanywa na Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Norway, ‘Norwegian Energy Agency’,NIBIO,YARA & NABA.
Serikali ya Norway imekuwa ikitekeleza miradi Mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Masuala ya Kilimo, Elimu, utafiti, Hali ya Hewa, mazingira, na kadhalika.
Aidha kupitia mkutano huo Serkali ya Norway imeahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania katika jitihada zake za kupambana athari za mabadiliko ya Tabianchi, uhifadhi na usimamizi wa Mazingira.