Na Mwandishi Wetu.
UJUMBE wa wataalaam 34 wa masoko ya mitaji kutoka Burundi umekiri kwamba sekta ya masoko ya mitaji ya Tanzania ni imara na ya kisasa, hivyo inawapa msingi mzuri wa kuijenga yao nchini mwao.
Ujumbe huo wenye watu 34 uko jijini Dar es Salaam kwa ziara ya mafunzo katika Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na kati yao watu 29 wamepitia programu mafunzo ya mtandaoni ya wiki sita kuhusu dhamana na uwekezaji, iliyoendeshwa kwa ushirikiano kati ya CMSA na Taasisi ya Dhamana na Uwekezaji ya London (CISI).Akizungumza Dk. Arsene Mugenzi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji ya Burundi ndio ameongoza ujumbe wa watu hao ambapo amesema soko la mitaji la Tanzania ni lenye uhai mkubwa ukilinganisha na masoko ya Afrika Mashariki, jambo ambalo lina mengi ya kutufundisha.
“Namna wanavyoendesha masoko ya mitaji hapa inatupa msingi wa kuijenga yetu wenyewe.Tanzania na Burundi ni marafiki wa karibu, na urafiki huo unaonekana hadi katika taasisi mbalimbali kati ya nchi hizo mbili.
“Lengo la ziara yetu ni kujilinganisha na kujifunza kutoka kwa Baraza la Masoko ya Mitaji (CMC) la Tanzania, ambalo lina uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika sekta hii, huku sisi tukiwa bado katika hatua za mwanzo za maendeleo. Ziara hii ni ya muhimu sana kwetu.
“Utendaji wao na mbinu za udhibiti zimetupatia maarifa ya msingi yatakayotusaidia kuanzisha mifumo sahihi ya kuboresha ufanisi wa masoko yetu ya mitaji,” ameongeza.
Kwa upande wake, Meneja wa Mawasiliano wa CMSA, Bw. Charles Shirima, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa mamlaka hiyo CPA. Nikodemus Mkama, amesema ushirikiano kati ya taasisi hizo mbili ni muhimu katika kubadilishana uzoefu ambao utawezesha ujenzi wa soko la mitaji imara la Afrika Mashariki.“Ushirikiano huu unalenga kujenga soko la mitaji la kikanda lenye viwango vya pamoja.”
Amefafanua wataalamu wa Burundi waliopitia programu ya wiki sita mtandaoni wamepata sifa inayoheshimika sana katika sekta ya masoko ya mitaji, kwani inathibitisha uwezo wao si tu ndani ya nchi yao, bali pia katika ngazi ya kikanda na kimataifa.
“Ndio maana ninahamasisha washiriki wengi zaidi kutoka taasisi zilizopata leseni, kama vile benki za biashara, kampuni za bima na mifuko ya hifadhi ya jamii, kushiriki mafunzo haya.Ninajivunia kueleza kuwa Februari, CISI ilichagua Tanzania kama eneo kuu kwa ajili ya ushirikiano huu Afrika Mashariki.
“ Hii inaonyesha si tu uwezo wa wataalamu wetu, bali pia uhusiano imara wa pande mbili kati ya Tanzania na nchi zingine za ukanda huu, kama Burundi. Mahusiano haya yamejengwa kupitia ushirikiano wa kiserikali na maono ya pamoja ya maendeleo ya kikanda,” aliongeza.
Ameongeza matumaini yake kuwa juhudi hizo ni mwanzo wa safari ya kuanzisha mfumo wa mafunzo na udhibiti wa masoko ya mitaji wa ndani ambao ni imara, endelevu, na unaofuata viwango vya kimataifa lakini ukibadilishwa kulingana na mazingira ya ndani.
Akieleza zaidi amesema mpango huo unakwenda sambamba na dhamira ya Tanzania ya kushiriki katika ushirikiano wa Afrika kuhusu kuunganisha masoko ya mitaji, hasa kupitia Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Mamlaka za Udhibiti wa Masoko ya Mitaji Afrika Mashariki (EASRA).
“Lengo ni kuhakikisha wataalamu wa soko hili wanapata mafunzo kulingana na viwango vya kimataifa. Mpango huo, unaoendeshwa kila mwezi Januari, unatoa chaguo la ushiriki wa ana kwa ana au mtandaoni. Baada ya kushiriki mafunzo, washiriki huendelea na vipindi vya mapitio na kujifunza kwa kina ili kujiandaa kwa matumizi ya vitendo katika sekta ya masoko ya mitaji.
“Sambamba na mpango wa vyeti, tumeanzisha pia Mpango wa Maendeleo Endelevu ya Kitaaluma (CPD). Kupitia mpango huu, kila mtaalamu aliyeidhinishwa anatakiwa kukamilisha idadi fulani ya saa za mafunzo kila mwaka kwa kawaida saa 35 ili kuwa na taarifa kuhusu mabadiliko ya kisheria, mitazamo mipya, na mbinu mpya za soko,” alieleza.
Amesema kwamba wanayo ratiba maalum ya shughuli za CPD na mfumo wa kufuatilia unaowasaidia wataalamu kurekodi saa zao na kuhakikisha wanaendelea kuwa sambamba na matakwa ya udhibiti. Ukuaji huo endelevu unahakikisha soko kuendelea kuwa imara, lenye maarifa, na linaloendana na viwango vya kimataifa,” alisisitiza.