Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dk. John Mduma, akizunguza na wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF wakati wa kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa hazina, WCF na TEF kilichofayika kwenye Hoteli ya Jada Morocco Square jijini Dar er Salaam Mei 15, 2025.
Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Ununuzi. Sabato Daudi Kosuri. akizungumza katika kikao kazi hicho.
…………..
Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Arusha. Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dk. John Mduma, amesema kuwa mfuko huo umefanya mabadiliko makubwa, yakiwemo kufuta madai ambayo walikuwa wanadai kutoka kwa waajiri wa sekta binafsi waliochelewesha kuwasilisha michango yao kwa wakati.
Dk. Mduma amesema kuwa kwa kipindi cha miaka minne iliyopita, kabla ya mabadiliko ya sheria, WCF ilikuwa ikitoza riba ya asilimia 10 kwa mwezi kwa michango iliyocheleweshwa, hali ambayo ilisababisha ongezeko kubwa la deni kwa waajiri.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam na wahariri kutoka Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), katika kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na WCF na TEF, Dk. Mduma alisema:
“Busara ilitumika katika Awamu ya Sita ambapo riba hiyo kubwa ilifutwa, na kubaki deni la msingi tu. Waajiri waliotakiwa kulipa walipewa msisitizo kulipa deni hilo la msingi pekee,” alisema.
Ameeleza kuwa, riba hiyo ya asilimia 10 kwa mwezi sasa imepunguzwa hadi asilimia 2 kwa mwezi, jambo alilolitaja kuwa ni nafuu kubwa kwa sekta binafsi.
Vilevile, Dk. Mduma alisema kuwa tangu Juni mwaka jana, WCF ilipata uthibitisho wa ubora wa huduma zake kwa viwango vya kimataifa (ISO certified), hatua iliyowafanya kuwa taasisi inayotambulika kimataifa kwa utoaji wa huduma bora.
“Wataalam wa kimataifa waliotupima walithibitisha kuwa tunakidhi viwango vya ubora. Hii inajenga imani kwa wadau wetu kuwa tumejidhatiti kutoa huduma zenye viwango vya hali ya juu. Kila mwaka wataendelea kutufanyia tathmini kuhakikisha tunazingatia viwango hivyo,” alisema.
Aidha, Dk. Mduma alisema kuwa kwa sasa WCF inatumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kwa zaidi ya asilimia 90 katika shughuli zake, ikiwemo usajili na upokeaji wa taarifa za ajali, hali inayoimarisha uwazi na ufuatiliaji wa huduma kwa wanachama.
Kwa upande wake, mmoja wa wanufaika wa mfuko huo, Bi. Imaculate Digula, mkazi wa Kigamboni, alieleza namna alivyofaidika na huduma za WCF baada ya mume wake aliyekuwa mfanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania kufariki dunia katika ajali ya gari mwaka 2021 wakati wa safari ya kikazi kutoka Arusha kwenda Tanga.
“Kwa kweli sikuwahi kusikia kuhusu WCF, lakini baada ya msiba, Benki Kuu walinieleza kuwa mume wangu alikuwa mwanachama wa mfuko huo na wao walikuwa wanamchangia. Nilipoenda kufuatilia, niligundua kuwa ni mfuko wenye huduma bora na wa kuaminika,” alisema Digula.
Aliongeza kuwa tangu mume wake afariki, WCF wamekuwa wakimhudumia kwa karibu, wakiwemo watoto wao wanne waliokuwa na umri chini ya miaka 18 wakati wa kifo cha baba yao.
“Mtoto wangu wa mwisho sasa yuko kidato cha kwanza. WCF wamekuwa wakitoa mafao ya kila mwezi kwa ajili ya watoto hadi wafikishe miaka 18. Pia wanafuatilia kama mtoto anaendelea na masomo. Huu ni msaada mkubwa kwa mjane kama mimi. Nawashukuru sana kwa kututhamini na kutusaidia baada ya janga hili,” alisema.