Viongozi wa taasisi zinazokopesha bila kuchukua amana wakiwa kwenye mafunzo


………………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kutoa elimu ya mfumo maalumu wa kuhakiki taarifa za wakopaji kabla ya kutoa mikopo kwenye taasisi zinazokopesha wananchi bila kuchukua amana.
Elimu hiyo ya siku mbili imetolewa jijini Mwanza ambapo watoa huduma zaidi ya 50 wa taasisi hizo kutoka Kanda ya ziwa wameweza kujengewa uwezo juu ya mfumo huo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya elimu hiyo wameishukuru BoT kwa namna inavyoendelea kuwalea katika misingi mizuri ya kutoa huduma huku wakiomba mafunzo hayo kuwa endelevu ili wazidi kujifunza zaidi na zaidi.
Aziza Hussein kutoka taasisi ya mikopo ya MSJ iliyoko mkoani hapa, amesema mafunzo hayo yatamsaidia kufanya kazi ya utoaji wa mikopo kwa ufanisi mkubwa kutokana na kuwa na taarifa za wateja wake.
Kwa upande wake Michael Faida kutoka kampuni ya microfinance iliyoko Mkoa wa Geita, amesema kabla ya mafunzo hayo walifanya kazi kwa hasara kutokana na wateja wengi kuchukua mikopo na kushindwa kurejesha kwa wakati.
“Kutokuwa na uelewa wa mfumo ilituathiri sana kwani tulitoa mikopo kwa wateja bila kujua taatifa zao,unakuta mtu amekopa sehemu kama tatu hivyo anakuwa na mikopo mingi ambayo inamshinda kurejesha lakini mfumo huu sasa utakuwa msaada mkubwa kwetu”, Alisema Faida
Naibu Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania Dkt. Ephraim Mwasanguti, amesema mfumo huo utawasaidia kujiendesha vizuri kwenye taasisi zao hivyo kupata faida na kupunguza mikopo chechefu.