Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Abdul Mhinte, amesema kuwa punda ana haki kama ilivyo kwa wanyama wengine, ikiwa ni pamoja na haki ya kutolala njaa, kutopata maumivu, kupata maji safi, na kuwa huru dhidi ya magonjwa pamoja na kazi zinazozidi uwezo wake.
Mhinte aliyasema hayo Mei 17, 2025, katika maadhimisho ya Siku ya Punda Duniani yaliyofanyika katika Kijiji cha Chambalo, Wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma.
Maadhimisho hayo yalifadhiliwa na Shirika la Brooke East Africa kupitia Shirika la INADES-Formation Tanzania na Shirika la Kutetea Haki za Wanyama (ASPA), kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Lengo lilikuwa kutoa elimu, matibabu na chanjo kwa zaidi ya punda 400.
“Punda ana haki ya kutopata majeraha au mateso wakati wa kazi, kupata mapumziko ya kutosha na kupewa hifadhi stahiki,” alisema Mhinte, akiwasisitizia wafugaji umuhimu wa kutambua mchango wa mnyama huyo katika maendeleo ya kiuchumi vijijini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Benezeth Lutege, alisema kuwa biashara ya punda na mazao yake ilisababisha kutoweka kwa wanyama hao barani Afrika. “Takwimu zinaonyesha kuwa punda milioni 5.9 walikuwa wanachinjwa kila mwaka hadi kufikia mwaka 2021. Ili kumnusuru, nchi za Afrika zilikubaliana kusitisha biashara hiyo kwa kipindi cha miaka 15,” alisema.
Katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi wa INADES-Formation Tanzania, Mbarwa Kivuyo, alisema wamekuwa wakisambaza elimu ya matunzo bora ya punda kwa wafugaji wa Chambalo. Elimu hiyo inahusisha umuhimu wa lishe bora, upole wakati wa kazi, matumizi ya matandiko ili kuzuia majeraha, na umuhimu wa mapumziko.
“Punda ni mnyama mwenye akili na huelewa maelekezo kwa haraka. Hahitaji kupigwa fimbo wala kuchapwa. Tunawaelimisha wafugaji kutumia lugha ya upole badala ya nguvu,” alisema Kivuyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, Juma Mnyika, aliongeza kuwa biashara haramu ya ngozi ya punda ilishamiri kati ya mwaka 2016 na 2022, na kusababisha idadi ya punda kushuka kutoka 12,611 hadi 8,228. Alipongeza serikali kwa hatua ya kupiga marufuku biashara hiyo, akisema imezuia kutoweka kwa punda nchini.
Lenard Saki, mfugaji wa punda kutoka Chambalo, alieleza jinsi elimu hiyo ilivyombadilishia mtazamo wake kuhusu mnyama huyo. “Niliamini punda ni mkorofi, lakini sasa nimejua anatakiwa kupendwa. Nilimpatia matibabu kwa upole na amepona haraka,” alisema.
Dkt. Charles Bukula, mtaalamu wa mifugo kutoka INADES-Formation Tanzania, aliwahimiza wafugaji kuhakikisha kuwa punda hawabebi mizigo mizito kupita kiasi. “Punda anatakiwa kubeba mzigo usiozidi theluthi moja ya uzito wake. Zaidi ya hapo ni kumnyanyasa,” alisisitiza.
Kwa ujumla, maadhimisho ya mwaka huu yameibua hamasa mpya ya kutambua nafasi ya punda katika jamii — si tu kama mnyama wa kazi, bali pia kama rasilimali muhimu ya kiuchumi inayohitaji kulindwa, kuthaminiwa na kuheshimiwa.