Dodoma
Tanzania imeendelea kuwa kinara katika usimamizi na uendelezaji wa Sekta ya Madini katika eneo la Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hali iliyoivutia nchi jirani ya Kenya kuja kujifunza mbinu bora za uchimbaji wa makaa ya mawe.
Ujumbe kutoka Wizara ya Nishati na Petroli ya Kenya, Mamlaka ya Nishati na Petroli, Idara ya Makaa ya Mawe, umewasili nchini kwa ziara ya mafunzo yenye lengo la kubadilishana uzoefu na kujifunza kutoka kwa mafanikio ya Tanzania katika sekta hiyo muhimu hususan uchimbaji na biashara ya Makaa ya Mawe.
Katika kikao kilichofanyika leo Mei 19, 2025, Jijini Dodoma, na kuongozwa na Kamishna Msaidizi wa Madini anayeshughulikia Uchimbaji Mdogo wa Madini, Francis Mihayo ambaye katika maelezo yake amesema kuwa shughuli za uchimbaji na biashara ya Makaa ya Mawe ni moja ya eneo ambalo Tanzania imefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Kamishna Mihayo ameueleza ujumbe huo kuwa mafanikio ya Tanzania katika kuratibu uchimbaji wa madini pamoja na makaa ya mawe ni yametokana na usimamizi thabiti wa Sekta ya Madini nchini sambamba na marekebisho ya Sheria ya Madini mnamo mwaka 2017.
“Katika miaka ya hivi karibuni Sekta ya Madini imekuwa ikifanya vizuri kutokana na Serikali kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji hapa nchini ikiwepo Makaa ya Mawe na tunashuhudia uchimbaji wa kibiashara unaozingatia sheria, taratibu na utunzaji wa mazingira,” amesema Mihayo.
Ujumbe wa Kenya ukiongozwa Kaimu Mkurugenzi wa Petroli nchini humo Robert Kibiwot umeonesha kufurahishwa na juhudi zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Madini katika kuimarisha sekta hiyo na kutoa mchango chanya kwa maendeleo ya uchumi wa nchi.
Akizungumza katika kikao hicho, Kibiwot amesema kuwa, Kenya ni moja ya nchi iliyojaaliwa kuwa na rasilimali ya Makaa ya Mawe lakini bado haijaanza kuchimbwa.
“Ni kweli tuna makaa ya mawe lakini bado hatujaanza kuchimba, tunaagiza makaa ya mawe kutoka Tanzania, Afrika Kusini na Marekani kwasasa, ndiyo maana tukaona tuje Tanzania kujifunza namna bora ya kuwesha kuvuna makaa ya mawe” amesisitiza Kibiwot.
Ziara hiyo inatarajiwa kujumuisha pia kutembelea Mgodi ya Makaa ya Mawe wa Kiwira unaomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa lengo la kuona kwa vitendo utekelezaji wa mikakati ya Serikali ya Tanzania katika sekta ya madini hususan makaa ya mawe.
Kwa miaka ya hivi karibuni, Tanzania imeweka mkazo mkubwa katika kuimarisha Sekta ya Madini, hatua ambazo zimeanza kuleta mafanikio makubwa katika sekta hiyo na kuvutia mataifa mengi kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara na hatimaye kuja kujifunza kuhusu usimamizi bora wa Sekta hiyo.