Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Mei 20,2025 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
Katika hatua ya kuimarisha upatikanaji wa huduma za kisheria kwa wananchi wa mijini na vijijini, Serikali kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) imeanzisha mfumo wa kidijitali wa eRITA, unaomwezesha mwananchi kutuma maombi ya nyaraka mbalimbali na kuzichukua kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya bila ya kuhangaika.
Akizungumza leo Mei 20, 2025 jijini Dodoma wakati wa kuwasilisha taarifa ya mafanikio ya miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro amesema kuwa mfumo huo ni sehemu ya juhudi za serikali katika kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kutumia teknolojia.
“Kwa sasa mwananchi anaweza kutuma maombi ya usajili wa vizazi, vifo, ndoa, talaka na udhamini kupitia mtandao na kupata nyaraka kwenye Ofisi ya Mkuu wa Wilaya bila kuhangaika,” amesema Dk. Ndumbaro.
Katika juhudi nyingine za maboresho, Waziri huyo alieleza kuwa Serikali imeongeza idadi ya Ofisi za Mashtaka za Wilaya kutoka 53 mwaka 2021 hadi kufikia 108 mwaka 2025. Vilevile, idadi ya watoa huduma wa utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala (ADR) imefikia 498, hatua inayolenga kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani.
Kwa upande wa elimu ya sheria, Dk. Ndumbaro amesema kuwa tangu mwaka 2021, jumla ya wataalamu 2,375 wa sheria wamehitimu kutoka Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo (Law School of Tanzania), huku wanafunzi 2,876 wakihitimu kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama kilichopo Lushoto.
“Tanzania inasimama imara kama mfano wa nchi zinazoendeleza haki, sheria na utawala bora kwa njia shirikishi na ya kidijitali,” amefafanua Dk. Ndumbaro.