Na, WAF-Dodoma.
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, ametoa muongozo akieleza kuridhishwa na majibu ya Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, kufuatia maswali ya nyongeza yaliyoulizwa na Mbunge wa Nanyumbu, Mhe. George Mwenisongole, kuhusu utekelezaji wa Sera ya Afya ya mwaka 2007 inayosisitiza huduma bure kwa wajawazito.
Spika Tulia ametoa muongozo huo leo Mei 20, 2025 Bungeni jijini Dodoma kufuatia swali la msingi la Mhe. Mwenisongole aliyetaka kufahamu kama Sera ya Taifa ya Afya ya mwaka 2007 bado ipo na inatekelezwa.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Mollel wakati akijibu swali hilo amesema sera hiyo bado ipo na inaendelea kutumika kutoa miongozo ya utoaji wa huduma za afya nchini huku akieleza kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za mapitio ya sera hiyo na kwamba kuanza kutumika kwa Bima ya Afya kwa Wote kutakuwa suluhisho la kudumu.
Katika maswali ya nyongeza, Mhe. Mwenisongole alidai kuwa licha ya uwepo wa sera hiyo, kwa uhalisia hakuna mama mjamzito anayejifungua bure, akieleza kuwa baadhi ya vituo vya afya na hospitali bado huwatoza kina mama, ikiwa ni pamoja na kuwaagiza kununua vifaa kama nyuzi, dripu na glavu vifaa ambavyo mara nyingine hubaki hospitalini bila kutumiwa. Alitaka kujua msimamo wa Serikali kuhusu hali hiyo.
Dkt. Mollel alieleza kuwa utekelezaji kamili wa huduma bure kwa wajawazito unahitaji bajeti kubwa ya takribani Shilingi Bilioni 227, wakati bajeti ya dawa kwa mwaka mzima ni Shilingi Bilioni 200 pekee. Hivyo, changamoto za kifedha huathiri utekelezaji kamili wa sera hiyo.
Aidha, ametaja kuwa baadhi ya matatizo yanayotokea yanatokana na changamoto za kiuongozi katika baadhi ya maeneo, akitolea mfano ziara waliyoifanya na Waziri Mkuu katika jimbo la Nanyumbu, walibaini matumizi mabaya ya rasilimali na fedha zilizokuwa hazitumiki licha ya hospitali kukosa dawa.
Kuhusu vifaa vinavyoletwa na wajawazito na kubaki hospitalini, Dkt. Mollel amesema suala hilo linahitaji kufuatiliwa kwa kina kwa kuwa linaweza kuwa linatokana na matatizo ya kiutawala au upungufu wa uwazi katika matumizi ya vifaa hivyo.
Baada ya majibu hayo, Spika Dkt. Tulia Ackson alieleza kuwa ameridhika kuwa majibu ya Naibu Waziri wa Afya yametolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 53 ya Bunge, ambayo inahusu utoaji wa majibu ya Serikali kwa maswali ya wabunge, na hivyo hakukuwa na haja ya kuendelea na mjadala zaidi kuhusu suala hilo.