Na Mwandishi wetu Jeshi la Polisi, Arusha
Jeshi la Polisi Mkoani Arusha kupitia operesheni iliyofanyika kuanzia mwezi Aprili mwaka huu hadi sasa limefanikiwa kuwakamata watumiwa 148 wa makosa mbalimbali ikiwemo ubakaji, ulawiti, dawa za kulevya na pombe ya moshi
Akitoa taarifa hiyo leo Mei 20, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amebainisha kuwa miongoni mwa waliokamatwa ni Watuhumiwa 29 kwa tuhuma za ubakaji na wengine 22 kwa tuhuma za ulawiti.
SACP Masejo amesema mara baada ya kufikishwa Mahakamani mtuhumiwa 01 alihukumiwa kwenda jela kifungo cha miaka 30 kwa tuhuma za ubakaji na Watuhumiwa wengine kesi zao zipo katika hatua mbalimbali Mahakamani.
Kwa upande wa dawa za kulevya Jeshi hilo lilifanikiwa kuwakamata Watuhumiwa 67 ambapo kati yao Watuhumiwa 29 walikamatwa wakiwa na Mirungi Kilogramu 969 na Watuhumiwa 22 wakiwa na bhangi kilogramu 22.3.
Kamanda Masejo amebanisha kuwa watuhumiwa hao wa Dawa za kuelvya tayari walifikishwa Mahakamani ambapo Watuhumiwa 04 walihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela, mtuhumiwa 01 kifungo cha miaka 20 na wengine kesi zao zipo katika hatua mbalimbali.
Pia kwa kipindi hicho walifanikiwa kukamata Watuhumiwa 30 wakiwa na pombe ya Moshi lita 210 na mitambo 09 ya kutengenezea pombe hiyo ambapo watuhumiwa wote tayari wameshafikishwa Mahakamani kwa taratibu za kisheria.
Aidha Jeshi la Polisi Mkoani humo limewataka baadhi ya watu wachache wanaojihusisha na vitendo vya kihalifu kuacha mara moja vitendo hivyo kwani litawakamata na kuwachukulia hatua za kisheria.