Meneja wa AUWSA mkoa wa Arusha ,Mhandisi Justine Rujomba akizungumza kuhusu mradi huo jijini Arusha



Happy Lazaro,Arusha .
Meneja wa AUWSA mkoa wa Arusha ,Mhandisi Justine Rujomba amesema kuwa,kumekuwepo na mafanikio makubwa ambayo yamepatikana kupitia utekelezaji wa mradi mkubwa wa maji wa thamani ya Shilingi Bilioni 520, unaofadhiliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Mhandisi Rujomba amesema kuwa, kupitia mradi huu, wameweza kujenga matanki 11 ya kuhifadhi maji, ambapo kwa sasa wana uwezo wa kuhifadhi lita milioni 40 kwa siku. Tenki kubwa lina ujazo wa lita milioni 10 na hata maji yakikatika, wanaweza kuendelea kutoa huduma kwa saa nane bila changamoto yoyote.
Akizungumzia upande wa majitaka, AUWSA imepanua mtandao wa ukusanyaji kutoka asilimia 8.03 mwaka 2020/21 hadi asilimia 39.5 mwaka 2024/25. Pia imenunua magari matano ya kunyonya majitaka yenye uwezo wa kubeba kati ya lita 5,000 na 10,000.
“Majitaka yanayokusanywa kutoka kwa wateja zaidi ya 10,930 yanatibiwa katika mabwawa ya kisasa yaliyopo Kata ya Terati, yenye uwezo wa kutibu lita milioni 22 kwa siku. Awali, mabwawa hayo yalikuwa na uwezo wa lita milioni 3.5 pekee,” amesema.
Rujomba alieleza kuwa muda wa upatikanaji wa huduma ya maji umeongezeka kutoka saa 16 mwaka 2020 hadi saa 22 mwaka 2025. Idadi ya wateja waliounganishwa na huduma za maji pia imeongezeka kutoka 71,183 mwaka 2021 hadi 134,000 kwa sasa.
P”amoja na mafanikio hayo, Biteko alieleza wasiwasi wake kuhusu kiwango kikubwa cha upotevu wa maji,” amesema Mhandisi Rujomba.
Ameongeza kuwa kuna umuhimu wa kushughulikia malalamiko ya wananchi kuhusu bili zisizoendana na matumizi.
“Mkiona wananchi wanalalamika kuwa bili ni kubwa kuliko matumizi, hilo ni jambo linalowahusu moja kwa moja. Hakikisheni mnalidhibiti,” amesisitiza.
Mhandisi Rujomba, amesema kuwa ,maeneo yanayohudumiwa na AUWSA ni pamoja na Jiji la Arusha, Monduli, Ngaramtoni, USA River, Mererani, na Longido – likijumuisha kata za Namanga na Kimokou – kwa jumla ya wakazi 1,076,523 kulingana na sensa ya mwaka 2022.
Mradi mkubwa uliofanyika unahusisha upatikanaji wa maji safi, uondoaji wa majitaka, na uimarishaji wa uwezo wa taasisi. AUWSA imejenga mtambo wa kutibu maji safi katika chanzo cha Midawe unaoweza kutibu lita milioni 10 kwa siku, ofisi kuu katika eneo la Safari City pamoja na ofisi nne za kanda.
“Kwa sasa tunaweza kusema AUWSA ndiyo mamlaka ya kwanza nchini yenye mabwawa bora na yenye uwezo mkubwa wa kutibu maji taka. Pia tumefanikisha kuchimba visima 56, viwili kati ya hivyo vikitoa maji kwa nguvu ya asili bila mashine – jambo linalosaidia wananchi kuendelea na kilimo hata visima hivyo vikiwa havifanyi kazi,” amesema Rujomba.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Mashaka Biteko, ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha (AUWSA) kwa hatua kubwa ya mafanikio katika utoaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira, baada ya kufanikisha upatikanaji wa huduma hiyo kwa asilimia 99.2 — zaidi ya lengo la Serikali la kufikia asilimia 95 ifikapo mwaka 2025.
“Fedha zilizowekwa hapa ni nyingi mno, zaidi ya bilioni 500. Ni lazima fedha hizi zitafsiri maisha bora ya watu. Maisha hayawezi kuwa bora kama hakuna maji. Maji hayana mbadala.”amesema Dkt.Biteko.
“Niwapongeze kwamba kiwango cha maji mnachozalisha ni kikubwa kuliko mahitaji, manake ni kwamba upatikanaji wa maji umefika asilimia 99. Hii ni hatua kubwa sana,” amesema Biteko.
Aidha, alihimiza umuhimu wa kuwa na vyanzo mbadala vya nishati, akieleza kuwa tatizo la umeme linaweza kuathiri moja kwa moja upatikanaji wa maji.
“Ikitokea umeme umekatika, backup yenu ni nini?” alihoji Biteko, ambapo Mkurugenzi Mtendaji wa AUWSA, Mhandisi Justine Rujomba, alieleza kuwa mamlaka hiyo ipo katika hatua za awali za kuandaa mazingira kwa wawekezaji binafsi kuwekeza katika mfumo wa nishati ya jua (sola).
“Lengo letu ni kuhakikisha kila kituo cha pampu kinakuwa na chanzo mbadala cha umeme ili kuondoa utegemezi wa gridi pekee,” amesema Rujomba.