Chuo Kikuu Mzumbe kimezindua Kituo cha Umahiri katika Ufundishaji na Ujifunzaji kwa Njia ya Mtandao (Talfsiri), ambacho kitawawezesha wanafunzi kujifunza wakiwa mbali bila kukumbwa na changamoto mbalimbali za kimazingira au muda.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, alisema kuwa kituo hicho kimewezeshwa kupitia fedha za Serikali chini ya Mradi wa HEET kupitia mradi huo, chuo kimepata studio ya kisasa itakayobadilisha mfumo wa jadi wa kufundisha darasani.
“Badala ya mwanafunzi kukaa darasani akisubiri kumskiliza mwalimu, sasa mwalimu ataweza kufundisha kwa njia ya masafa na kumfikishia mwanafunzi maarifa popote alipo,” alisema Prof. Mwigoha.
Aliongeza kuwa hatua hiyo itaongeza ufanisi wa ufundishaji, kupanua wigo wa wanafunzi wanaoweza kufikiwa, na pia kusaidia chuo kuongeza udahili na mapato kwa ujumla.
“Tunawaomba wadau mbalimbali wa Chuo Kikuu Mzumbe kutumia kituo hiki kwa ajili ya kazi mbalimbali za kitaaluma ili kuongeza tija na ufanisi zaidi,” alisisitiza Prof. Mwigoha.
Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Shule ya Utawala wa Umma na Menejimenti, Dkt. Idda Lyatonga, alieleza kuwa kabla ya kuwa na kituo hicho, walimu walikumbwa na changamoto nyingi za kurekodi vipindi, ikiwa ni pamoja na kufanya kazi hizo wakiwa majumbani, hali iliyosababisha matatizo ya sauti na usumbufu wa kelele.
“Kwa sasa, kupitia kituo hiki, walimu wanafanya kazi kwa ufanisi zaidi. Vipindi vinarekodiwa bila usumbufu wa kelele za nje, hali inayorahisisha kujifunza kwa wanafunzi, hasa wale wanaofanya kazi na kusoma kwa pamoja (graduate students). Wanaweza kusoma wakiwa sehemu yoyote bila kulazimika kuwepo darasani,” alisema Dkt. Lyatonga.
Naye Mratibu wa Mradi wa Kujifunza na Kufundishia kwa Mtandao katika Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Perpetua Kalimasi, alisema kuwa kituo hicho kitajikita katika kuongeza uwezo wa wanataaluma katika matumizi ya teknolojia ya kisasa katika ufundishaji.
Alibainisha kuwa kituo hicho kitatoa msaada kwa wanafunzi katika matumizi ya mifumo ya kujifunzia kwa njia ya mtandao, hivyo kuwawezesha kusoma popote walipo alimradi wana mtandao.
“Lengo ni kwenda sambamba na maendeleo ya teknolojia ya kidijitali katika sekta ya elimu, na kuhakikisha mbinu mpya za ufundishaji zinamfikia mwanafunzi popote alipo,” alifafanua Dkt. Kalimasi.