Rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mheshimiwa Thabo Mbeki ameshiriki mhadhara wa Siku ya Afrika uliofanyika katika Ukumbi wa Nkrumah wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Akizungumza katika mjadala huo Mhe.Thabo Mbeki amesema mjadala huo umewakutanisha wasomi, vijana na Taasisi ya Thabo Mbeki ili kuangalia kwa pamoja juu ya nini kifanyike ili kuiletea maendeleo Afrika.
Mhe. Mbeki alielezea hali ya sasa ya Afrika kwa kutumia muktadha wa kihistoria wa ukoloni, udhaifu wa taasisi za ndani, utegemezi mkubwa wa mataifa ya nje na haja ya Umoja wa Afrika na Taasisi zake kufikia malengo ya kuanzishwa kwake..
“Kesho ya bara la Afrika haiwezi kuendelea kuamuliwa na watu wengine bali utatokana na uamuzi, juhudi na mshikamano wa Waafrika wenyewe na sio watu wengine”, alisema.
Alisema kuwa licha ya mafanikio ya kisiasa yaliyopatikana baada ya uhuru, bado Afrika inakumbwa na changamoto za kiuchumi, usalama, na ukosefu wa mshikamano
Ametoa wito kwa Nchi za Afrika kuhakikisha umoja na mshikamano unaendelea kuwepo na kuongeza kuwa taasisi za Umoja wa Afrika na Tume ya AU lazima zihakikishe zinasimamia misingi ya kuanzishwa kwao na kutimiza malengo yao
Ameongeza kuwa vyama vya siasa katika bara la Afrika vinahitaji viongozi kama Mwalimu Nyerere watakao iwezesha Afrika kufikia matarajio yake ya kiuchumi na kisiasa.
Ametoa rai kwa vijana wa vyuo vikuu kushirikiana na vijana wenzao barani Afrika na kutumia nafasi zao kutoa muelekeo wa nini kifanyike ili kufufua matumaini na mwelekeo wa bara la Afrika.
Nao Wasomi wa UDSM wakichangia mjadala huo, wamesema ni wakati wa kuchukua hatua na kuacha kulalamika na kushirikiana kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kweli kwa bara la Afrika
Akitoa salamu za shukurani baada ya mhadhara huo Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete ameishukuru Taasisi ya Thabo Mbeki kwa kukichagua Chuo hicho kuwa mwenyeji wa mhadhara wa Siku ya Afrika kwani unaonesha imani ya Taasisi hiyo kwa Chuo hicho.
Amesema kauli mbiu ya mhadhara wa Siku ya Afrika usemao “Hali ya Bara la Afrika:Ufufuo mpya wa Mwamko wa Kiafrika“ unaakisi mahitaji ya kweli ili kuifanya Afrika iendelee.
Mhadhara huo uliwakutanisha wasomi kutoka UDSM na Taasisi ya Thabo Mbeki kwa lengo la kujadili na kujenga uelewa wa pamoja, huku wakitafakari makosa yaliyopita na kutathmini hatua stahiki zinazopaswa kuchukuliwa ili kuleta maendeleo ya kweli barani Afrika.
Mhadhara huo uliwaleta pamoja wasomi, wanafunzi, viongozi wa serikali, na wanadiplomasia ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Afrika ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Mei.
Washiriki wa mhadhara kwa pamoja walitafakari hatma ya bara la Afrika katika muktadha wa changamoto na fursa zinazolikabili bara la Afrika.