Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chan’ga akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 22, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akitoa mwelekeo wa utabiri wa hali ya hewa kipindi cha msimu wa kipupwe unaotarajia kuanza mwezi Juni hadi Agosti 2025
………
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa mwelekeo wa hali ya hewa kipindi cha msimu wa kipupwe unaotarajia kuanza mwezi Juni hadi Agosti mwaka huu, ambapo Kutakuwa na upepo wa wastani utakaovuma kutoka Kusini Mashariki kwa maeneo mengi ya Nchi pamoja na vipindi vichache vya upepo mkali utakaovuma kutoka kusini hususan mwezi Juni na Julai 2025 katika maeneo ya Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya nchi kavu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 22, 2025 Jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chan’ga, amesema kuwa katika kipindi hicho vipindi vya mvua za nje ya msimu vinatarajiwa katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria hususan Mikoa ya Kagera, Geita na Mwanza, Simiyu na Mara.
Dkt. Chan’ga amesema kuwa pia kutakuwa na mvua za nje ya msimu ukanda wa Pwani na maeneo ya nchi kavu (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Mtwara, Lindi, Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba).
”Kipindi cha msimu wa kikupwe joto la bahari katika eneo la kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (kusini mwa Madagascar) linatarajiwa kuwa la juu ya wastani, hali hii inatarajiwa kudhoofisha mgandamizo mkubwa wa hewa katika eneo hilo na hivyo kupunguza kasi ya upepo wenye baridi kutoka kusini kuelekea katika maeneo ya nchi yetu” amesema Dkt. Chan’ga.
Amesema kuwa kutakuwa na vipindi vichache vya upepo unaovuma kutoka msitu wa Congo kuelekea maeneo ya Magharibi mwa nchi, hali hiyo inatarajiwa kuimarisha mifumo isababishayo mvua kwa baadhi ya nyakati hususan katika maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria.
Dkt. Chan’ga amesema kuwa athari zinazoweza kutokea katika msimu wa kipupwe ni pamoja na magonjwa yanayohusiana na hali ya baridi kama vile homa ya mapafu na magonjwa ya mifugo yanaweza kujitokeza, hususan maeneo ya magharibi mwa nchi, nyanda za juu kusini magharibi na baadhi ya maeneo kwa kiasi kidogo.
“Kutakuwa na vumbi linalosababishwa na upepo katika baadhi ya maeneo linaweza kupelekea uwepo wa magonjwa ya macho na magonjwa mengine yanayohusiana na hali hiyo, Upungufu wa maji na malisho unaweza kujitokeza katika baadhi ya maeneo” amesema Dkt. Chan’ga.
Dkt. Chan’ga ametoa tahadhari za kiafya zichukuliwe ili kulinda jamii dhidi ya magonjwa yanayoweza kusababishwa na baridi na vumbi.
Amesema kuwa kutokana na hali ya ukavu inayotarajiwa katika maeneo mengi katika kipindi hicho, maji na malisho yanapaswa kutumika kwa uangalifu ili kupunguza athari zinazotarajiwa.
Amewashauri wafugaji kuendelea kuzingatia ratiba za kuogesha mifugo ili kudhibiti magonjwa ya mifugo na kufuata ushauri wa wataalam.
“Wakulima wanashauriwa kulima mbogamboga na mazao ya mizizi kama vile viazi katika maeneo oevu na pia katika maeneo yanayotarajiwa kupata vipindi vya mvua katika kipindi hiki cha msimu wa Kipupwe” amesema Dkt. Chan’ga.
Amesema kuwa watumiaji wa baharini wanashauriwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa zikiwemo utabiri wa kila siku, angalizo na tahadhali ili kuongeza ufanisi na usalama wa shughuli za baharini, na kupunguza athari za upepo mkali unaotarajiwa. Hata hivyo, sekta za ujenzi, madini na uchukuzi zinatarajiwa kunufaika kutokana na hali ya hewa inayotarajiwa.
TMA imetoa angalizo la kuendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na kutoa mrejesho, huku watumiaji wa taarifa za utabiri wa hali ya hewa wanashauriwa pia kufuatilia na kuzingatia utabiri wa saa 24, siku 10, mwezi pamoja na tahadhari za hali mbaya ya hewa kama zinavyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
MATARAJIO YA VIWANGO VYA JOTO – Katika kipindi cha msimu wa Kipupwe (JJA) 2025,hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi.
Hata hivyo, hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Singida pamoja na maeneo ya magharibi mwa mkoa wa Dodoma. Aidha, vipindi vya baridi zaidi vinatarajiwa kujitokeza katika mwezi Julai.
Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Mwanza, Mara, Geita, Kagera, Shinyanga na Simiyu) – Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi. Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10 oC na 18 oC.
Ukanda wa pwani ya kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba)- Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi.
Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto16oC na 24oCkwa maeneo ya mwambao wa pwani na visiwani na kati ya nyuzi joto 12oC na 20oC katika maeneo ya nchi kavu. Hata hivyo, maeneno yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 12oC.
Nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara) – Hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo mengi. Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10 oC na 20 oC.Hata hivyo, maeneo yenye miinuko yanatarajiwa kuwa na kiwango cha nyuzi joto chini ya 10 oC.
Kanda ya magharibi (Mikoa ya Tabora, Katavi na Kigoma) – Hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo mengi ambapo joto la chini linatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10⁰C na 18⁰C.
Kanda ya kati (Mikoa ya Singida na Dodoma) – Hali ya baridi ya wastani hadi baridi kali inatarajiwa katika maeneo mengi ya mkoa wa Singida na magharibi mwa mkoa wa Dodoma. Hata hivyo, hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi inatarajiwa katika maeneo ya mashariki mwa mkoa wa Dodoma. Kiwango cha joto la chini kinatarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 10oC na 20oC.