Serikali ya Tanzania imetajwa kuwa mshirika muhimu katika mafanikio ya kampuni ya kimataifa ya Puma Energy, huku nchi ikitajwa kuongoza kwa mapato na faida kati ya nchi zote zinazohudumiwa na kampuni hiyo barani Afrika.
Akizungumza Mei 26, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa ziara ya uongozi wa kampuni hiyo katika ofisi za Hazina, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alisema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano wa kimkakati kati ya Serikali na wawekezaji binafsi. Alibainisha kuwa Puma Energy inamilikiwa kwa asilimia 50 na Serikali ya Tanzania, na asilimia nyingine 50 ni ya wawekezaji binafsi.
“Ushirikiano huu ni wa kimkakati kwa maendeleo ya sekta ya nishati nchini. Tutaendelea kufanya mageuzi ya kiutendaji na kuhakikisha matumizi bora ya rasilimali kwa manufaa ya Taifa,” alisema Mchechu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy duniani, Marc Russel, alisema Tanzania ni eneo lenye fursa nyingi, na akapongeza utayari wa Serikali kushirikiana na wawekezaji kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi.
Naye Mkurugenzi wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah, alisema Tanzania inaongoza kwa mafanikio miongoni mwa mataifa yote yanayohudumiwa na Puma. Alieleza kuwa kampuni hiyo ina dhamira ya kuendelea kuwekeza nchini kwa lengo la kukuza uchumi na kuboresha huduma kwa wananchi.