Taasisi ya nishati mbadala ya REEP imezindua Mradi wa Pure Growth Fund kwa lengo la kuwawezesha wananchi, hasa walioko katika sekta za kilimo na uvuvi, kupata teknolojia za kisasa zitakazosaidia kuhifadhi mazao, kupunguza upotevu na kuongeza thamani ya uzalishaji.
Uzinduzi huo umefanyika wakati ambapo takwimu zinaonesha kuwa asilimia 50 ya mazao ya kilimo na uvuvi hupotea kuanzia hatua za awali hadi kufika sokoni, hali inayochangiwa na uelewa mdogo na ukosefu wa teknolojia licha ya juhudi za serikali kupunguza changamoto hizo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkazi wa REEP, Philemon Msuya amesema kuwa mradi huo umebuniwa ili kuunga mkono jitihada za serikali katika kuwawezesha wazalishaji wa ndani kufanikisha malengo yao ya kujikwamua kiuchumi.
Aidha, mradi huo wenye thamani ya euro milioni 2.5 umeweka mkazo kwa wakulima na wavuvi wadogo na wa kati, kwa kuwawezesha kuongeza uzalishaji na kufikia masoko kwa ufanisi zaidi.
PICHA ZOTE NA JAMES SALVATORY TORCH MEDIA