Na Prisca Libaga RAS Arusha
Wanafunzi zaidi ya 800 kutoka shule za msingi mkoani Arusha, wamejitokeza kwa wingi kushiriki kwenye mashindano ya mchujo kwa ajili ya kupata timu ya mkoa itakayoshiriki mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya taifa, yatakayofanyika mkoani Iringa.
Mashindano haya ya mchujo yamefanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Ilboru, yakilenga kuchagua kikosi bora kitakacholiwakilisha mkoa wa Arusha, ambao mwaka jana uliibuka mshindi wa kwanza kitaifa. Wanafunzi walionekana kuwa na ari kubwa na matumaini ya kuendeleza rekodi hiyo ya ushindi.
Aidha Mgoka Saimon, Mratibu wa Michezo Wilaya ya Ngorongoro, alieleza kuwa lengo kuu la mchujo huo ni kupata timu yenye ushindani mkubwa itakayotoa changamoto kwa mikoa mingine. Aliongeza kuwa mafanikio ya mwaka jana yanatoa msukumo mkubwa kwa wanafunzi kushiriki kwa bidii.
Miongoni mwa wanafunzi walioshiriki mchujo huo ni Regine Jacob Selemani na Goodfrey Joseph, ambao walionyesha matumaini ya kushinda tena:
“Tunaamini tunaweza kushinda kama mwaka jana. Tunajituma sana mazoezini na tunataka kuipeperusha vyema bendera ya mkoa,” alisema Goodfrey.
Kwa upande wa walimu kutoka Wilaya ya Monduli, ambae pia ni Afisa Michezo wa Monduli alisema maandalizi yanaendelea vizuri huku wakieleza ubora wa wanafunzi hasa wale walio chini ya umri wa miaka 14.
“Tuna vijana wenye vipaji vikubwa na tunawaandaa kimwili na kiakili kwa ushindani wa kitaifa.”
Naye Msafiri Saidi, mwalimu alisisitiza kuzingatiwa kwa nidhamu na ushindani wa hali ya juu. Tuna matarajio makubwa na tunaamini wataliwakilisha vyema mkoa wetu.”
Mashindano haya yanachukuliwa kama sehemu muhimu ya kukuza vipaji vya michezo mashuleni, huku yakitoa fursa kwa wanafunzi kuonyesha uwezo wao kitaifa. Mkoa wa Arusha una matumaini makubwa ya kutetea ubingwa wake kwa mwaka huu.