
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Afrika Kusini (DBSA), Bi. Buitumelo Mosako, baada ya kukamilisha mazungumzo yao yaliyojikita kujadilki namna ya kuendeleza ushirikiano kati ya Tanzania na Benki hiyo, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) iliyofanyika, Abidjan nchini Ivory Coast
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Abidjan)
Na Benny Mwaipaja, Abidjan
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika Kusini (DBSA), kwa kushiriki katika ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), mradi ambao ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania na nchi jirani zitakazonufaika na mnyororo wa thamani wa mradi huo wa kikanda.
Mhe. Dkt. Nchemba amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bi. Buitumelo Mosako, kando ya Mikutano ya Mwaka ya Bodi ya Magavana wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) iliyofanyika, Abidjan nchini Ivory Coast.
“Tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa Benki ya Maendeleo ya Afrika Kusini (DBSA) kwa mchango wenu muhimu katika kufadhili ujenzi wa SGR kipande cha 3 na 4 (Makutupora hadi Isaka) kwa kiasi cha dola za Marekani milioni 100. Zaidi ya hapo, tunatambua na kuthamini msaada wa kifedha wa kiasi cha dola milioni 100 uliotolewa awali kwa ajili ya kujenga kipande cha 2, ambao uliweka msingi imara kwa mradi mzima wa SGR” alisema Dkt. Nchemba
Alisema kuwa kutokana na juhudi hizo za pamoja, maendeleo ya ujenzi yamekuwa makubwa ambapo kipande cha 1 (Dar es Salaam hadi Makutupora) kimekamilika kwa asilimia 99.63 na treni imeanza kufanya kazi rasmi Julai 2024, wakati kipande cha 3 (Makutupora hadi Tabora) ujenzi wake umefikia asilimia 14.53, na kipande cha 4 (Tabora hadi Isaka) kimefikia asilimia 6.48.
“Bi. Boitumelo Mosako, kutokana na umuhimu wa mradi huu, nachukua fursa hii tena kuiomba benki yako iendelee kuunga mkono utekelezaji wa kipande cha 6 na 7 ya Reli ya Kisasa (SGR), ambavyo upatikanaji wake wa fedha za kutekeleza vipande hivyo unasimamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Aliongeza kuwa Tanzania imefungua milango ya ushiriki wa sekta binafsi katika kuendesha mradi huo wa kimkakati ikiwemo uwekezaji wa mabewa na vichwa vya treni na kutoa wito kwa wawekezaji kuchangamkia fursa hiyo.
Aidha, Mhe. Dkt. Nchemba aliishukuru Benki hiyo kwa kuonesha utayari wake wa kutaka kuwekeza zaidi katika maendeleo ya Tanzania katika sekta za elimu, maji, afya, ujenzi wa miundombinu pamoja na kilimo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya DBSA, Bi. Buitumelo Mosako, alisema kuwa milango ya ushirikiano na Tanzania iko wazi na kwamba Benki yak eina subiri kukamilika kwa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 ili waweze kuangalia maeneo ya kushirikiana.
Alisisitiza kuwa Benki yake iko tayari kuwekeza zaidi Tanzania katika kusaidia miradi ya kimkakati na kijamii katika sekta za m aji, afya, nishati, uchumi wa kidigitali, ujenzi wa makazi ya gharama nafuu na ujenzi wamiundombinu mbalimbali.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Katibu Msaidizi wa Baraza la Mawaziri, Bw. Fidelis Mkatte, Kamishna wa Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade, Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Deni la Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justine, pamoja na maafisa wengine waandamizi kutoka Serikali ya Tanzania.