NA DENIS MLOWE IRINGA
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kanda ya kati, imeendelea kutoa Elimu ya Matumizi ya nishati safi ya kupikia ya gesi mkoani Iringa, lengo likiwa ni kuhamasisha matumizi ya nishati safi pamoja na kuimarisha usalama katika usambazaji wa nishati hiyo.
Akizungumza Katika Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Veta mkoani hapa ,Meneja wa EWURA kanda ya kati,Hawa Lweno, na kuwahusisha kada mbalimbali wakiwemo mama lishe,waendesha pikipiki na wasambazaji wa gesi ya kupikia mkoani Iringa amewataka kuhakikisha wanazingatia viwango vya usalama katika usambazaji wa gesi (LPG) ili kulinda maisha na mali za wananchi.
Alisema lengo la Ewura ni kuhakikisha watumiaji wa gesi ya kupikia wanazingatia masuala ya usalama, afya na utunzaji wa mazingira pamoja na kuhakikisha watoa huduma tunaowadhibiti wanafuata na kutii masharti ya leseni zao.
Aidha aliongeza kuwa moja kati ya majukumu ya Ewura ni kuhakikisha kuwa wannatatua migogoro baina ya watumiaji huduma pamoja na watoaji huduma, kutoa leseni na vibali mbalimbali.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Iringa, Adofu Kimea, ameeleza kuwa licha ya takwimu za majanga ya moto mkoani Iringa kuwa ndogo, bado kuna haja ya kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na wasambazaji ili kuzuia majanga yanayoweza kuepukika.
Naye, Wakala wa Vipimo, mkoa wa Iringa Richard Kimario, amewasihi mawakala wa gesi kuhakikisha wanakagua mitungi kabla ya kuiingiza sokoni ili kuepusha changamoto za upungufu wa gesi na kuhakikisha uzito wa gesi unalingana na viwango vilivyowekwa.
Hata hivyo Mafunzo hayo yamepokelewa kwa furaha na washiriki, ambao wameeleza kuwa yatawasaidia kuboresha huduma zao na kulinda usalama wa jamii.