Afisa Huduma kwa Wateja Mkoa wa Temeke, Bw. Goodluck Assenga (aliyeshika maiki) akitoa ufafanuzi kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Bw. Ismail Ali Ussi kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia majiko janja yanayotumia umeme, wakati alipotembelea Banda la TANESCO katika hafla ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru iliyofanyika leo Juni 1, 2025 katika Viwanja vya TANESCO Wilaya ya Yombo, Dar es Salaam.
Afisa Huduma kwa Wateja TANESCO Wilaya ya Yombo Bi. Angela Kalambo akitoa elimu kwa Mama Lishe na Baba Lishe kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia majiko janja yanayotumia umeme, wakati alipotembelea Banda la TANESCO Mkoa wa Temeke katika hafla ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru iliyofanyika leo Juni 1, 2025 katika Viwanja vya TANESCO Wilaya ya Yombo, Dar es Salaam.
Picha za matukio mbalimbali.
…………
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Bw. Ismail Ali Ussi, amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke kwa kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia majiko janja yanayotumia umeme.
Akizungumza leo, Juni 1, 2025, jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea Banda la TANESCO katika hafla ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru iliyofanyika katika Viwanja vya TANESCO Wilaya ya Yombo, Bw. Ussi amesema kuwa ni muhimu kwa jamii kutumia nishati safi ya umeme kwani ni rafiki kwa afya na mazingira.
“Majiko janja yanayotumia nishati ya umeme ni rafiki wa mazingira na yanatumia Unit chache za umeme. Nimeridhishwa na utekelezaji wa miradi yote katika Manispaa ya Temeke, ni muhimu kuwajibika katika utekelezaji wa miradi ili kufikia malengo ya maendeleo,”
amesema Bw. Ussi.
Kwa upande wake, Afisa Huduma kwa Wateja Mkoa wa Temeke, Bw. Goodluck Assenga, amesema kuwa majiko hayo yanaweza kutumika majumbani na katika maeneo ya biashara kama vile hoteli, kwani ni salama kwa mazingira na afya ya watumiaji. Huku akitoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa ya kununua majiko hayo sanifu.
Baadhi ya wananchi waliotembelea banda la TANESCO, akiwemo Bi. Mwanaidi Msuya na Bw. Edward John, wamelishukuru Shirika hilo kwa kutoa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia
Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2025 umebeba kaulimbiu isemayo: “Jitokeze Kushiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025 kwa Amani na Utulivu.” Wilaya ya Temeke wameupokea Mwenge huo kutoka Mkoa wa Lindi.