Na Silivia Amandius.
Kagera, Bukoba.
Katika kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Shirika la TEKLA limeandaa tukio maalum la kugawa msaada wa vifaa mbalimbali kwa watoto wenye ulemavu mkoani Kagera, ikiwa ni ishara ya upendo, kujali na kuthamini haki za watoto wote.
Tukio hilo limefanyika katika viwanja vya Gymkhana, likihudhuriwa na viongozi wa serikali, wazazi pamoja na wadau mbalimbali wa ustawi wa jamii. Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Kanali Mstaafu Hamis Maiga, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kanali Maiga alilipongeza Shirika la TEKLA kwa mchango wake mkubwa kwa jamii, akisema kuwa hatua hiyo ni ya kuigwa na kuungwa mkono na mashirika na watu binafsi.
“Kuwajali watoto wenye ulemavu ni kuenzi utu, kuleta usawa wa fursa na kuchangia maendeleo ya taifa letu. Watoto wote wanapaswa kuthaminiwa,” alisema Kanali Maiga.
Mkurugenzi wa TEKLA, Bi. Annalise Leonard Lubago, alisema kuwa tukio hilo limelenga kuhamasisha upendo na mshikamano kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu, hususan kipindi hiki cha kuelekea Juni 16 – Siku ya Mtoto wa Afrika.
“Watoto hawa wanahitaji mazingira rafiki, msaada wa vifaa na sauti ya matumaini. Dhamira yetu ni kuhakikisha hawabaki nyuma katika safari ya maendeleo,” alieleza Bi. Annalise.
Wazazi na walezi wa watoto walionufaika na msaada huo walionesha furaha na kutoa shukrani kwa TEKLA pamoja na serikali kwa kutambua kundi hilo maalum, wakisema msaada huo umeleta faraja na thamani kwa maisha ya watoto wao.
Baadhi ya vifaa vilivyotolewa ni pamoja na baiskeli za miguu mitatu, vifaa vya shule, sabuni na mavazi, vyote vikielekezwa kwa watoto wenye ulemavu.
Shirika la TEKLA limeendelea kuwa mstari wa mbele katika kusaidia makundi maalum kupitia misaada ya kijamii, elimu na uhamasishaji, kwa lengo la kujenga jamii jumuishi na yenye fursa kwa wote.
Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika mwaka huu yamebeba kaulimbiu inayohimiza usawa, ulinzi na fursa kwa watoto wote – wakiwemo wenye ulemavu.