Mawakala Usafirishaji wanawake wamekiri kukutana na vitendo vingi vya unyanyasaji wa Kingono kutoka kwa mameneja,Askari wabarabarani na wamiliki wa vyombo vya moto katika makampuni wanayofanyia kazi na kisha kuzitaka mamlaka za serikali hususani Polisi na Takukuru kuchunguza vitendo hivyo na kuwachukulia hatua wahusika.
Katika mafunzo ya wiki moja yenye lengo la kujengea uwezo madereva na mawakala usafirishaji maarufu makondakta kuhusu masuala ya sheria,kanuni,maadili pamoja usalama barabarani yaliyoratibiwa na chuo cha elimu ya biashara nchini(CBE) kwa kushirikina na mamlaka ya udhibiti wa usafiri ardhini(LATRA),Washiriki akiwemo Tenesia Rodwell wamesema mafunzo hayo yamewafungua macho kwani wanawake wamekuwa wakikumbana vitendo vingi vya ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kulazimishwa mapenzi na mabosi wao hivyo mamlaka za kiserikali zinapaswa kutupia jicho eneo hilo
Kwa upande wake Rehema Kaduma amezungumzia changamoto wanazokutana nazo wanawake kutoka kwa askari wa usalama barabarani ambapo amesema kuna wakati kama ulikuwa na mahusiano nae kimapenzi,ukichana nae anakuweka katika mazingira magumu ya kazi kwa kukupiga faini kila wakati.
Mara baada ya kusikia changamoto hizo ndipo wakufunzi kutoka chuo cha elimu ya biashara CBE akiwemo Dr Beny Mwenda na Jeremia Tumain ambae ni mkurugenzi wakatoa elimu juu ya hatua wanazopaswa kuchukua pindi wanapokutana na vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kuripoti polisi,LATRA ama kwenye taasisi nyingine za kiserikali.
Ukiachana na suala la ukatili ,Wakufunzi kutoka LATRA na jeshi la polisi kitengo cha usalama barabarani nao akiwemo Sajini Vicent Jingu askari wa Kitengo cha usalama barabarani amehimiza maadili na usafi wawapo kazini ili kuvutia wateja wao huku Yoyce Zakaria Nungwa afisa mfawidhi wa LATRA Njombe akitaka watu wote walio kwenye mnyororo wa sekta ya usafirishaji kuzingatia sheria na kanuni za usafirishaji.
Nae Katibu wa usafirishaji mkoa wa Njombe Zabron Mdemu ameipongeza serikali na wadau wote waliofanikisha zoezi hilo la mafunzo kwa madereva na makondakta kwani linawaongezea uelewa na kisha kuitaka jamii kutambua kazi hiyo na kazi kama kazi nyingine.