Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, akiagana na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ALSTOM, nchini Tanzania, inayojihusisha na uwekezaji katika ujenzi na uendeshaji wa miundombinu ya reli duniani, Bi. Kefilwe Mothupi, baada ya kumalizika kwa kikao kilichofanyika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, akiteta jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), Bw. David Kafulila, baada ya kumalizika kwa kikao na Ujumbe kutoka Kampuni ya ALSTOM, kilichofanyika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini, Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bw. Elijah Mwandumbya, akiongoza kikao na ujumbe wa Kampuni ya ALSTOM, ambapo pamoja na mambo mengine walijadiliana kuhusu uendelezaji wa miundombinu jijini Dar es Salaam, kikao hicho kilifanyika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini, Dodoma.
Mkurugenzi wa Miradi na Fedha, Ofisi ya ALSTOM, Bi. Julie Morel, akifanya wasilisho kuhusu utekelezaji wa mradi wa miundombinu jijini Dar es Salaam wakati wa kikao na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, kilichofanyika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini, Dodoma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma).
…….
Na. Josephine Majura, WF, Dodoma
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bw. Elijah Mwandumbya, amekutana na kufanya mazungumzo na Ujumbe kutoka Kampuni ya ALSTOM, yenye Makao yake Makuu nchini Ufaransa, iliyoonesha nia ya kuwekeza katika ujenzi na uendeshaji wa miundombinu ya reli ili kupunguza msongamano wa magari na kuboresha usafiri katika jiji la Dar es Salaam.
Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square, jijini, Dodoma na kuhudhuriwa na Kaimu Kamishna wa Kitengo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) Wizara ya Fedha, Bw. Bashiru Taratibu, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), Bw. David Kafulila, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Sheria, Wizara ya Fedha, Bi. Zawadi Maginga pamoja na wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Kampuni ya ALSTOM.