NAIBU Waziri Mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania na Waziri wa nishati,Dkt Dotto Biteko akifungua maonesho hayo jijini Arusha
Happy Lazaro,Arusha .
NAIBU Waziri Mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania na Waziri wa nishati,Dkt Dotto Biteko ameielekeza Wizara ya Maliasili.na utalii kutumia fursa za ukuaji wa sekta ya TEHAMA katika utangazaji utalii na upatikanaji wa masoko ya utalii kwa ushirikiana na mamlaka mbalimbali za Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara za utalii nchini ili kuchochea na kuvutia uwekezaji zaidi.
Ameyasema hayo jijini Arusha wakati akifungua onesho la utalii la kimataifa la Karibu -Kilifair 2025 linalofanyika kuanzia juni 6 hadi 8 katika viwanja vya magereza vilivyopo jijini Arusha .
Dkt.Biteko ambaye aliwamwakilisha Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania ,Dkt .Samia Suluhu Hassan amewataka pia
Kuendelea kubuni njia mbalimbali za uendelezaji wa mazao ya utalii nchini kwa kuzingatia mgawanyiko wa aina ya mazao na mtawanyiko wa kijiografia wa nchi yetu.
Aidha ametoa rai pia kwa Sekta Binafsi kuendelea kuwekeza katika sekta ya utalii, hususan katika eneo la huduma za malazi, ili kukidhi ongezeko la mahitaji ya soko hasa tukizingatia uwepo wa matukio mbalimbali ya kimataifa yatakayofanyika nchini kadhalika na mwitikio chanya wa watalii kutoka katika masoko yetu ya kimkakati na yale yanayokua kwa kasi Duniani.
“Napenda Niwahakikishie kwamba,Serikali itaendelea kushirikiana nanyi wadau katika nyanja mbalimbali kuhakikisha ustawi wa biashara za utalii nchini na maendeleo ya sekta kwa ujumla wake.”amesema Dkt.Biteko.
Ameongeza kuwa,Kauli Mbiu ya Onesho la KARIBU-KILIFAIR kwa mwaka 2025 ni “Utalii Endelevu, Kujenga Ustahimilivu na Ubunifu” hususan katika kipindi hiki ambacho sekta ya utalii imerejea katika hali yake ya ustawi baada ya kutokea kwa changamoto ya UVIKO-19, kauli mbiu hii imeakisi malengo yetu ya kisera katika kukuza utalii endelevu yaani Sustainable tourism, kama ambavyo imekuwa ikitiliwa mkazo na Shirika la Utalii Duniani (UN-Tourism).
Amesema kuwa, kauli.mbiu hiyo inaenda sambamba na azma yetu ya kukuza na kuendeleza sekta ya utalii nchini kwa kuimarisha ubunifu katika kutangaza vivutio na kutanua wigo wa mazao ya utalii, kusimamia matumizi endelevu ya rasimilmali za utalii, na kujenga uchumi jumuishi kwa jamii zetu na Taifa.
Amefafanua kuwa, onesho la KARIBU-KILIFAIR linaendelea kukua Kimataifa na kuvutia idadi kubwa ya washiriki, ambapo huwakutanisha wadau wa utalii kwa ajili ya kuwaunganisha kibiashara, kubadilishana uzoefu katika biashara za utalii na masoko ikiwemo pia, kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta hii muhimu ya kiuchumi.
“Nimejulishwa kuwa kwa mwaka huu pekee, onesho hili limewakutanisha waoneshaji zaidi ya 500 kutoka Tanzania Bara, Zanzibar na zaidi ya nchi 10 Duniani, wanunuzi wa kimataifa 1,000 kutoka zaidi ya mataifa 40, pamoja na maelfu ya wadau na wataalamu wa sekta ya utalii,hii inadhihirisha kuwa, dunia inaiangalia Tanzania na Afrika Mashariki kama kitovu cha utalii kinachokua kwa kasi, kilicho tayari na chenye kuaminika.”amesema Dkt.Biteko .
Aidha amefafanua kuwa,pamoja na mafanikio hayo sekta hiyo imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika uhifadhi wa maliasili na malikale, ustawi wa jamii na ukuaji wa kiuchumi. Mfano, takwimu mbalimbali zinaonesha kuwa, sekta hii inachangia asilimia 17.2 ya Pato Ghafi la Taifa (GDP) na asilimia 25 ya mauzo ya nje.
“utalii ni biashara inayofunganisha huduma, vivutio mbalimbali vikiwemo, mandhari ya kuvutia na ukarimu wa Watanzania, ikisimulia hadithi ya kipekee ya urithi wa kitamaduni na uvumbuzi wa kisasa ambapo makundi mbalimbali ya wageni hupata fursa ya kuvinjari na kufurahi.”amesema .
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, ameiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kulitambua eneo la Magereza – Kisongo kama eneo maalum kwa ajili ya maonesho ya kimataifa ya utalii ili kuvutia wageni kutoka mataifa mbalimbali.
Aidha ameshauri muda wa maonesho hayo uongezwe kutoka siku 3 hadi siku 5 au 7 ili kutoa fursa zaidi kwa wawekezaji kuonesha bidhaa na huduma zao, hasa zinazohusiana na mnyororo wa thamani katika sekta ya utalii.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya KARIBU-KILIFAIR Promotion, Dominic Shoo amesema onesho hilo ni daraja la kikanda na ulimwengu katika kukuza utalii kutoka ndani na nje ya nchi.
Shoo amesema onesho hilo limeshirikisha waonyeshaji zaidi ya 800 na wanunuzi zaidi ya 1000 ambao ni wanunuzi wa ndani na wa kimataifa kutoka nchi zaidi ya 40 pamoja na makampuni ya utalii zaidi ya 500 yameshiriki maonesho hayo
Aidha ameiomba serikali kuendelea kushirikiana na waandaaji wa onesho hilo ili lukuza utalii, ikiwemo kuvuta mawakala wa utalii wa ndani na nje ya nchi katika kuhakikisha fursa za utalii zilizopo nchini zinakuwa kwa kasi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa masoko na biashara kutoka kampuni ya RSA Harveer Bhamra ,akizungumza mbele ya Dkt Biteko alipotembelea banda lao amesema kuwa, wana kiwanda kipo Moshi walikuwa na mashine lakini sasa hivi wameagiza mashine nyingine kwa ajili ya kufanyia kazi zao kwani wamechukua tender katika nchi ya Uganda,Kenya ,Malawi ,Angola na Congo .
Amesema kuwa,wanatengeneza magari Afrika nzima sio lazima Tanzania yenyewe na wanapeleka katika nchi mbalimbali ikiwemo ,Malawi , Congo na Dubai kwani wana mkataba nao katika kufanya kazi .
“Nakushuru sana Mhe kwa kutembelea banda letu na kuweza kujionea shughuli mbalimbali tunazozifanya kwani tumekuwa tukifanya kazi nzuri sana na tuna masoko ndani na nje ya nchi kwani wateja wetu wanatuamini kutokana na huduma nzuri tunazotoa “amesema Bhamra.


Mkurugenzi wa masoko na biashara kutoka kampuni ya RSA Harveer Bhamra akitoa maelezo kuhusu huduma wanazotoa kwa Naibu Waziri Mkuu wa jamhuri ya muungano wa Tanzania na Waziri wa nishati,Dkt Dotto Biteko alipotembelea kwenye banda lao jijini Arusha

