Katika kuadhimisha miaka 25 ya kuwaunganisha Watanzania, Vodacom Tanzania PLC imezindua kampeni kubwa ya kitaifa inayobeba ujumbe wa “Tupo Nawe, Tena na Tena.” Kampeni hii itakayodumu kwa miezi minne, kuanzia Juni hadi Oktoba 2025, inalenga kusherehekea safari ya mafanikio tangu walipoanza kutoa huduma nchini mnamo mwaka 2000 hadi leo.
Vodacom inawakumbusha Watanzania kuwa ipo nao sambamba katika kila hatua ya maisha yao, kutoka kipindi cha mawasiliano ya simu za kawaida hadi zama hizi za dijitali za M-Pesa, 5G, huduma za afya mtandaoni, elimu kwa njia ya simu na biashara za kidijitali.
“Miaka 25 ya Vodacom siyo tu kuhusu teknolojia; ni kuhusu mahusiano tuliyojenga na maisha ya Watanzania tuliyoyagusa. Kupitia ‘Tupo Nawe, Tena na Tena,’ tunawashukuru Watanzania kwa kutuamini na kutufanya kuwa mtandao wa mawasiliano unaoaminiwa na watu wengi zaidi nchini. Hali kadhalika, tunawaahidi kuwa bado tupo na tutaendelea kuwa nanyi kwa miaka mingi ijayo,” alisema Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Bw. Philip Besiimire.
Akiongelea mafanikio mbalimbali ya kampuni hiyo, Besiimire alisema kwamba walianzisha huduma ya M-Pesa mnamo mwaka 2008, ambapo imeleta mapinduzi katika sekta ya fedha nchini na kuchangia ujumuishi wa kifedha. Hali kadhalika kupitia mtandao wao ulionea nchi nzima na 5G ya kwanza Tanzania, Vodacom inaendelea kuwaunganisha Watanzania na kuwawezesha kushiriki katika ulimwengu wa kidijitali.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara wa kampuni hiyo Bi. Brigita Shirima aliongeza kwamba kupitia kampeni hii, Vodacom itaingia mtaani kuwasogezea karibu zaidi huduma wateja wake.
“Kampeni hii itaendeshwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani ambapo kutakuwa na msafara maalum utakaohusisha utoaji zawadi kwa wateja mitaani na katika maduka yetu makubwa, mauzo ya simu janja za kisasa, kutambua mawakala na wabia wetu wa biashara, WiFi ya bure, burudani tele pamoja na kushirikisha wafanyakazi wetu katika shughuli za kijamii kupitia programu maalumu ya Siku 25 za Upendo, zitakazowagusa wananchi moja kwa moja,” aliongeza Bi Shirima.
Kwa kumalizia, Bi Shirima pia aliwasihi wateja wa Vodacom na Watanzania kwa ujumla kushiriki kwenye kampeni hii ya kipekee, inayowaenzi wao kama nguzo kuu ya mafanikio ya Vodacom, kwa sababu bila wao, mafanikio haya yasingewezekana.
Katika kuadhimisha miaka 25, Vodacom inaahidi kuendelea kutoa huduma za viwango vya juu kwa wateja wao zaidi ya milioni 28 kama inavyoripotiwa katika takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano nchini TCRA.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC, Phillip Besiimire (wa pili kushoto) akiwa na Ofisa Utumishi Mkuu wa kundi la makampuni Vodafone Leanne Wood (katikati), Mkurugenzi wa M-Pesa, Epimack Mbeteni na Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara Brigita Shirima (kulia) wakipeperusha bendera kuashiria maandamano wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 25 ya Vodacom Tanzania katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaamtarehe 10 Juni 2025.