NA DENIS MLOWE, IRINGA
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry William Silaa amezindua rasmi maabara tano za TEHAMA katika shule tano za sekondari mkoani lringa zilizotokana na juhudi za mbunge wa viti maalum Mkoa wa Iringa Ritah Kabati.
Akizungumza katika hafla iliyofanyika katika Shule ya Sekondari Nyalumbu, iliyoko wilayani Kilolo , Waziri Jerry Slaa alizindua maabara hizo tano katika shule za Shule za Sekondari Kilolo, Udzungwa, Selebu, Uhambingeto na Nyalumbu zenye kompyuta mpakato 20 kwa kila shule.
Waziri Silaa alisema kuwa kitendo cha mbunge Rittah Kabati kwa juhudi alizofanya kuziwezesha shule 5 kuwa na vifaa vya TEHAMA vilivyowezesha kuanzishwa kwa maabara hizo vimetolewa kupitia ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la Reneal International Education Outreach ni jambo la kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo nchini.
Alisema kuwa juhudi za Kabati na ushirikiano wa shirika hilo unaonesha namna sekta binafsi inavyoweza kushirikiana na Serikali katika kuleta mageuzi ya kidijitali, hususan kwa vijana wetu walioko mashuleni.
Waziri Silaa aliongeza kuwa Wizara anayoiongoza ndiyo yenye dhamana ya kusimamia masuala ya TEHAMA nchini, na kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), inatekeleza miradi mbalimbali inayochagiza ukuaji wa TEHAMA, hususan katika sekta ya elimu ambayo ina uhitaji mkubwa sana wa masuala ya kiteknolojia.
Aidha, Waziri ameuagiza Mfuko wa UCSAF kuhakikisha walimu wa TEHAMA katika shule hizo wanapatiwa mafunzo maalum ya TEHAMA, ili kuwawezesha kutumia programu mbalimbali katika komputa.
Aliongeza kuwa Serikali chini yw Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuweka mkazo kwenye maendeleo ya TEHAMA ikiwa ni pamoja na upanuzi wa miundombinu ya Internet nchini katika ngazi za 4g ili kuwaongezea wanafunzi uwezo wa kujifunza kwa kufanya tafiti mtandaoni na hivyo kuboresha uwezo wao kitaaluma.
Alitumia nafasi hiyo kumpongeza mbunge wa viti maalum kwa uthubutu wake wa kujitoa katika kusaidia jamii hususani sekta ya elimu hivyo jamii inatakiwa kumuunga mkono.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Iringa, Ritha Kabati ambaye ameseidia kupatikana kwa kompyuta hizo kupitia wafadhili amesema msaada huo ni mchango wake katika kuunga mkono juhudi za Serikali kutoa elimu bora kwa vitendo katika upande wa TEHAMA.
Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Kilolo, Rebecca Msemwa akitoa shukrani kwa mbunge Kabati alisema kuwa ni jambo la kuungwa mkono na jamii nzima kwa kitendo cha kujitoa kwa jamii katika kuwaletea maendeleo hasa katika suala la teknolojia.
Alisema zamani alikuwa anakutana na komputa chuoni ila kwa serikali ya Mama Samia masomo ya TEHAMA unalkutana nayo mapema hali ambayo itawawezesha wanafunzi kusoma masomo ya TEHAMA na kutaleta mabadiliko chanya kwenye sekta ya elimu.







Matukio mbalimbali ya uzinduzi