Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb.) ameisisitiza kampuni ya Hunan ER-Kang ya nchini China kuongeza uzalishaji wa dawa za binadamu katika kiwanda chake kilichopo Dar es Salaam, Tanzania.
Msisitizo huo umetolewa wakati Mhe. Waziri Kombo alipotembelea Makao Makuu ya Kampuni hiyo yaliyopo jijini Changsha, China na baadae kufanya mazungumzo na uongozi wa kampuni hiyo yaliyoangazia mikakati ya kupanua kiwanda na kuongeza uzalishaji nchini.
Akifafanua jitihada za Serikali ya Tanzania katika kuboresha huduma ya afya kwa wananchi, Waziri Kombo ameeleza kuwa upatikanaji wa dawa za kutosha kwa ajili ya wananchi ni sehemu ya kipaumbele katika utekelezaji wa majukumu wa sekta ya afya.
Ameongeza kuwa, ni wakati sahihi kwa kampuni hiyo kuongeza uzalishaji wake nchini ambao utaipunguzia Serikali mzigo wa kununua dawa nje ya nchi na kuongeza kuwa ziada ya dawa itakayozalishwa na kampuni hiyo itasambazwa katika nchi 16 za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kufuatia Tanzania kushinda zabuni ya kusambaza dawa katika nchi wanachama wa jumuiya hiyo kupitia Bohari ya Dawa (MSD).
Amesisitiza kuwa jukumu hilo linahitaji upatikanaji wa uhakika wa dawa na vifaa tiba na kwamba hiyo ni fursa adhimu kwa kampuni hiyo kutumia ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na China ili kukuza biashara yake kimataifa.
Aidha, Waziri Kombo ameihakikishia kampuni hiyo ushirikiano wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao nchini na kwamba Wizara itaendelea na jukumu lake la msingi la uratibu wa masuala ya kimataifa kwa kushirikiana na sekta mama katika kufanikisha uwekezaji huo.
Naye Mwenyekiti wa Kampuni ya ER-Kang, Bw. Fangwen Shuan ameahidi kupanua kiwanda na kuongeza uzalishaji wa dawa za binadamu nchini. Vilevile, ameeleza nia ya kampuni hiyo kuwekeza katika uzalishaji wa chuma na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo hususan korosho, karanga na ufuta.