Meneja Msaidizi wa Mradi wa BRT-3, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Rottoson Kabalika, ( wa kwanza kushoto) akiwa katika eneo la Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Tatu (BRT-3) akitoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali kwa watejaji wa Mamlaka ya Barabara nchini Malawi kuhusu utekelezaji wa mradi huo katika ziara iliyofanyika leo Juni 12, 2025 jijini Dar es Salaam.
Wafanyakazi wa Mamlaka ya Barabara nchini Malawi wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa TANROADS wakati walipotembelea Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Tatu (BRT-3).
…………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Barabara nchini Malawi imeipongeza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa utekelezaji mzuri wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Tatu (BRT-3), unaoanzia Posta hadi Gongo la Mboto, ambao kwa sasa umefikia asilimia 90 ya utekelezaji.
Pongezi hizo zimetolewa kufuatia ziara ya wafanyakazi wa Mamlaka ya Barabara Malawi nchini Tanzania kwa lengo la kujifunza namna bora ya utekelezaji wa miradi ya usafiri wa haraka, ili kuongeza ufanisi katika sekta ya miundombinu nchini mwao.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyofanyika leo Juni 12, 2025 jijini Dar es Salaam, Meneja Msaidizi wa Mradi wa BRT-3 kutoka TANROADS, Mhandisi Rottoson Kabalika, amesema kuwa ujio wa watendaji hao kutoka Malawi unalenga kujifunza mbinu bora za utekelezaji wa mradi kwa kuzingatia viwango vya ubora.
Mhandisi Kabalika amesema kuwa mradi huo umezingatia matumizi jumuishi kwa watumiaji wote wa barabara, ikiwa ni pamoja na watembea kwa miguu na vyombo vyote vya usafiri, ili kuhakikisha usalama na ufanisi wa huduma.
“Wageni wetu wamekuja kuona mradi huu kwa ukaribu. Tumewaonyesha maeneo mbalimbali kuanzia hatua za awali za ujenzi hadi hatua za mwisho, ikiwemo vituo vya mabasi vinavyojengwa katikati ya barabara,” amesema Mhandisi Kabalika.
Kwa mujibu wa Mhandisi Kabalika, mradi wa BRT-3 unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 30, 2025, na mara baada ya kukamilika, utakabidhiwa kwa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) kwa ajili ya kuanza kutoa huduma.
Kwa upande wake, Kiongozi wa msafara kutoka Malawi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Barabara wa Mamlaka ya Barabara Malawi, Bw. Robson Piringu, amesema kuwa Malawi ina mpango wa miaka mitano wa kuimarisha miundombinu ya barabara na hivyo waliona ni muhimu kujifunza kutoka TANROADS.
“Tunashukuru uongozi wa TANROADS kwa kutupa taarifa sahihi na ushirikiano mkubwa. Tumejifunza mambo mengi, ikiwemo ushirikiano kati ya TANROADS, Mkandarasi na Mkandarasi Mshauri, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya mradi huu,” amesema Bw. Piringu.
Naye Mkandarasi Mshauri wa Mradi wa BRT-3, Mhandisi Hendrush Nyange, ameeleza kuwa mradi huo uko katika hatua za mwisho, huku akifafanua kuwa asilimia kubwa ya vifaa vya ujenzi vimetoka ndani ya nchi, jambo linalochochea uchumi.
Ameeleza kuwa licha ya changamoto zilizojitokeza katika hatua mbalimbali za ujenzi, juhudi za pamoja kati ya TANROADS, Mkandarasi na Mkandarasi Mshauri zimesaidia kuzikabili na kuendelea kusonga mbele.
Mradi wa BRT-3 unatekelezwa kwa kutumia zege, na unakadiriwa kudumu kwa zaidi ya miaka 30 kabla ya kuhitaji maboresho madogo. Utekelezaji wa mradi huo unasimamiwa na TANROADS na unafadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Serikali ya Tanzania.