Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
Mbunge wa viti maalum Mkoani Pwani, Subira Mgalu, amemkabidhi Mwenyekiti wa UWT Taifa,Mery Chatanda gari aina ya Noah kwa ajili ya Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT)Bagamoyo ikiwa ni jitihada za kuimarisha utendaji kazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia jumuiya hiyo.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano ya gari hilo, Mgalu amesema kuwa utekelezaji huo ni sehemu ya nadhiri aliyojiwekea awali ya kuhakikisha UWT inapata chombo cha usafiri ili kurahisisha shughuli za kila siku za jumuiya.
Ameongeza , gari hilo linapaswa kutumika pia kama nyenzo ya kuimarisha kampeni na kuhamasisha wananchi, hasa wanawake, kumchagua tena Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwakumbusha wananchi kazi zilizofanyika katika maeneo yao.
“Ilikuwa imani yangu kutekeleza hili, Nashukuru mwenyezi mungu kanijaalia leo kulitimiza kwa ajili ya Jumuiya na Chama” anasema Mgalu .
Wakati wa kupokea gari hilo, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mery Chatanda, amempongeza Mgalu kwa moyo wake wa kujitolea kwa jumuiya hiyo.
Chatanda amekabidhi gari hilo kwa wilaya ya Bagamoyo na kuwataka viongozi wanalisimamia na kuhakikisha linatumiwa kwa malengo yaliyokusudiwa ili kusaidia kurahisisha shughuli za utendaji wa jumuiya.


